TRA kuanza kuwabana wasiotoa risiti, kudai

20Jul 2021
Daniel Sabuni
ARUSHA
Nipashe
TRA kuanza kuwabana wasiotoa risiti, kudai

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuanza  kutumia sheria katika kutoa adhabu kwa wale  wote watakaokaidi kutoa au kudai risiti kwa kuwa wamekuwa wakichangia upotevu wa mapato ya Serikali  hali inayodidimiza uchumi na  kukosa maendeleo ya nchi.

Baadhi ya wafanyabiashara wa jiji la Arusha wakifuatilia mkutano wao na Mamlaka ya mapato Tanzania uliomalizika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC.

Kamishina Mkuu wa TRA,  Alphayo Kidata ametoa taarifa hiyo, katika mkutano TRA na   walipakodi  jijini  Arusha wakiwemo wafanyabiashara pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali.

"Kuanzia sasa tutatumia sheria zetu kutoa adhabu kali kwa wale wasiotoa risiti ni vizuri tuwe na utamaduni wa kudai risiti kwani endapo utabainika itachukuliwa hatua kali,"amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela akizugumza katika mkutano huo, amewataka wakazi wa Mkoa wa Arusha kushirikiana katika kufichua biashara ya bidhaa bandia ambazo zimekuwa zikichangia kudidimiza uchumi.

"Bado mkoa wetu unatumika kama daraja la bidhaa za kughushi kwa  hiyo sisi kama Mkoa wa Arusha tunatakiwa kushirikiana na kuendelea kuhamasisha kuepuka kufanya biashara za bidhaa za kughushi,"amesema.

Mmoja wa washiriki  wa mkutano huo Kelvin Remen amesema mkutano huo ni  jukwaa muhimu litakalowasaidia wafabishara kulipa kodi kwa njia rafiki bila kuwa na matatizo yeyote kwa wafanyabiashara.