TRA wadai chanzo kushuka mapato

13Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Bukoba
Nipashe Jumapili
TRA wadai chanzo kushuka mapato

WAFANYABIASHA na wawekezaji wa ndani mkoani Kagera, wameilalamikia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani hapa kuwadhalilisha hivyo kusababisha kushindwa kuchangia mapato.

Wakizungumza kwenye kikao cha wadau wa kodi wa mkoa kilichowashirikisha wasimamizi wa kodi na walipakodi, baadhi ya wafanyabiashara hao walisema mfumo unaotumiwa na baadhi ya maofisa wa TRA katika kudai kodi umesababisha uadui mkubwa baina ya makundi hayo mawili.

Wakala wa kampuni ya Mukwano, Remigius Patrick, alisema kumekuwapo tabia ya baadhi ya maofisa wa TRA kuwajenga hofu walipakodi  na  kuonekana kutokuwa na imani nao  kulingana na hatua zinazochukuliwa na mamlaka hiyo.

Patrick  alisema hatua hizo zimefanya baadhi yao kukwepa kodi kwa kufanya biashara zingine kupitia wajasiliamali au njia isiyo rasmi  na kuhama mkoa na hatimaye kusababisha kupeleka mapato mikoa mingine.

"Wengi hukata tamaa za kufanya uwekezaji ndani ya mkoa huu kutokana na changamoto wanazokumbana nazo na kuamua kukimbilia sehemu yenye unafuu," alisema Patrick. 

Pia alisema kumekuwa na tozo nyingi na ucheleweshaji wa ukaguzi wa mzigo kwa muda mrefu kwa vigezo vya kutokuwa na vitambulisho.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Chai Kagera, Peter Mgimba, alisema kutokuwapo mazingira rafiki kati ya wafanyabiashara na TRA husababisha kuhamisha kodi na kupata mapato kidogo.

Mgimba alisema elimu kwa mlipakodi kabla ya kudai kodi itolewe mijini na vijijini kusaidia mwananchi wa mkoa huo kulipa kodi ndani mkoa wake na si kufuata bidhaa nje ya mkoa kufanya uwekezaji huko.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Adam Ntoga, alisema lengo la kukusanya mapato kwa mwaka jana ilikuwa Sh. bilioni 25.47 lakini yaliyokusanywa ni Sh. bilioni 24.3 pekee.
 
Alisema mamlaka imepanga kuongeza mapato kupitia madini, uvuvi, misitu, kilimo na ufugaji, sekta ambazo zilikuwa hazichangii mapato ya mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho, alisema ulipaji kodi husaidia maendeleo ya mkoa na taifa hivyo ni lazima kuwe na uhusiano mzuri kati ya watoza kodi na walipakodi.

Habari Kubwa