TRA yafunguka maswali ‘kigongo’ usaili ajira zao

03Sep 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
TRA yafunguka maswali ‘kigongo’ usaili ajira zao
  • *Ni yale yaliyoumiza vichwa waombaji 30,000

HATIMAYE Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefafanua kuhusiana na maswali matano ya usaili kwa walioomba ajira kwao na kuzua mijadala mikali kwenye mtandao kwa madai kuwa ni magumu na hivyo huenda wengi wakaishia kuambulia patupu.

Miongoni mwa maswali hayo yaliyosambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kudaiwa kuwa ‘kigongo’ mbele ya waombaji walio wengi, ni yale yaliyohoji kuhusu mapendekezo tisa yaliyotolewa hivi karibuni na Kamati Teule ya Rais iliyochunguza kuhusu usafirishaji kwenda nje wa mchanga wa madini (makinikia).

Akizungumza na Nipashe jana baada ya kuulizwa kuhusu maswali hayo, ambayo yalidaiwa kuwakumba waombaji 30,000 walioitwa kwa usaili kutoka miongoni mwa 56,000 waliojitokeza kuwania nafasi 400 zilizotangzwa, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Umma wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alisema Mamlaka hiyo haihusiki na maswali hayo na hivyo waulizwe wanaohusika.

“Hivi umesoma vizuri kichwa cha yale maswali? Kama kweli ungekisoma usingeuliza kama maswali yale yalitungwa na TRA… kasome vizuri maana utaona kabisa maswali yake yametoka wapi,” alisema Kayombo.

Kichwa cha habari kwenye maswali hayo ambacho Kayombo alisisitiza mwandishi akakisome, kilionyesha kuwa maswali hayo yameandaliwa na  Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira.

Aidha, karatasi hiyo yenye maswali iliandikwa juu kuwa maswali hayo ni mahojiano kwa waomba kazi wanaotaka nafasi za kuwa maofisa forodha daraja la pili TRA.

Alipoulizwa kuhusu maswali hayo jana, Naibu Katibu wa Kitengo cha Udhibiti na Ubora (PO-PSRS), Humphrey Mniachi, alisema: “Nipo tayari kukupa taarifa kwa undani zaidi kwa nini tumeuliza maswali haya… naomba nikukaribishe ofisini, nitakupa majibu ya uhakika,” alisema.

MASWALI YENYEWE
Picha mbalimbali zilizokuwa zikiwaonyesha maelfu ya vijana wakisongamana kuingia kwenye ukumbi wa usaili wa Shule Kuu ya Elimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE) zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mjadala kwa kuonyesha pia maswali hayo matano ‘kigongo’ kwa waliohudhuria usaili.

Miongoni mwa mijadala kwenye mitandao ilihoji uhusiano wa maswali na nafasi za kazi zilizotangazwa TRA.

Baadhi ya maswali hayo, ni pamoja na la kwanza lililohoji kuhusu Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDG) uliomalizika 2015 na kuwataka watahiniwa kuelezea SDG ni nini na kuorodhesha angalau malengo nane ya SDG’s.

Swali la pili liliuliza kuhusu Sheria ya Elektroniki na Mawasiliano ya Posta (306) kuhoji juu ya uamuzi wa serikali kuweka sheria hiyo katika kukuza uchumi wa taifa na swali la tatu, lenye vipengele vinne, lilihoji kuhusu masuala ya fursa za mkataba wa biashara baina ya nchi za Afrika na Marekani (AGOA).

Akizungumzia maswali hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya Utawala na Rasilimali Watu, alisema kwa mtazamo wake, aliona maswali yaliyoulizwa ni tofauti na ajira yenyewe na kwamba huenda lengo kuu lilikuwa ni kupunguza waombaji waliojitokeza kwa maelfu kulinganisha na nafasi zilizopo.

“Usahili wa kuandika maswali umeshapitwa na wakati. Maswali yanayopima uwezo wa kisaikolojia, kufikiri au uwezo wa kukubaliana na hali ngumu na uadilifu haya ndiyo yanatumika na dunia ya leo,” alisema Dk. Bana.

Habari Kubwa