TRA yatangaza kugawa makontena ya Makonda

12Oct 2018
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
TRA yatangaza kugawa makontena ya Makonda

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema imekamilisha utaratibu wa kugawanya mali zilizoko kwenye makontena ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na wiki ijayo zitaanza kutolewa.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, alisema hayo jana kwa njia ya simu alipoulizwa na Nipashe juu ya hatua zitakazofuata baada ya makontena hayo kukosa wateja na maombi ya taasisi mbalimbali kupewa vifaa hivyo.

Juzi, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Martin Busungu, aliomba serikali kuwapatia samani zilizozuiwa bandarini kwa ajili ya jengo la Shule ya Sekondari Kawawa iliyoko Mafinga mkoani Iringa, inayomilikiwa na kikosi cha 841KJ Mafinga.

“Kwa sasa siko ofisini lakini nimeacha watu wanamalizia utaratibu. Mali hizo zitagawanywa kwenye taasisi mbalimbali nchini baada ya utaratibu kukamilika. Wiki  ijayo nitakuwa katika nafasi nzuri ya kueleza zaidi,” alisema.

Alipoulizwa juu ya taasisi zitakazogawiwa samani hizo, alisema: “Tutaweka hadharani, hayo maombi ya JKT nami nimeona kwenye WhatsApp pia, ila wenzangu wanakamilisha taratibu fulani na kama tulivyosema toka awali baada ya mnada wa tatu, zitagawanywa.”

Septemba 2, mwaka huu, Kamishana huyo alizungumza na Nipashe na kueleza kuwa Septemba 8 ni mnada wa mwisho kwa mujibu wa sheria ya forodha ambayo inataka mnada kufanyika mara tatu.

Wakati huo alipoulizwa ni kwanini yanakosa wateja, Kichere alisema: “Hata sisi tunashangaa kwa nini hakuna wateja wakati bei tuliyopanga ni ya kawaida kabisa ambayo inaendana na mali husika na inatuwezesha kupata kodi ya serikali.”

“Wateja wengi hawafiki bei tuliyopanga, hivyo sheria inataka mnada kufanyika mara tatu na inaposhindikana basi tutafuata hatua nyingine. Lakini tunaamini kabisa bei tuliyoweka ni sahihi kabisa,” alifafanua.

Aidha, aliwataka Watanzania kujitokeza kununua mali hizo na kwamba hadi sasa kati ya makontena 20 hakuna hata moja lililopata mteja na kwamba kwenye mnada wa mwisho watu wajitokeze kununua kwa wingi.

Mnada wa kwanza wa makontena hayo yaliyoko katika bandari kavu ya DCID ulifanyika Agosti 24, mwaka huu, na Jumapili iliyofuata mmiliki wake alifanya ibada kanisani kutaka wateja wakosekane na atakayenunua atalaaniwa na Mungu.

Baada ya kauli ya kiongozi huyo kutoa kauli hiyo, Waziri Fedha na Mpango, Dk. Philip Mpango, alifanya ziara ya kushtukiza kwenye bandari hiyo na kutaka mnada kuendelea bila kujali kauli za kiongozi huyo kwa kuwa anatakiwa kulipa kodi kama Watanzania wengine kwa kuwa ni mali binafsi.

Aidha, siku chache baadaye, Rais Dk. John Magufuli alifunga mjadala kwa kusema ni lazima kiongozi huyo alipe kodi na kwamba mali hizo zilichanganywa na za wafanyabiashara kwa ajili ya kuuzwa kwenye maduka yao.

 

Alisema walimu hawajasema wanahitaji makochi au masofa na kwamba kati ya kontena hizo mbili au tatu ndiyo za walimu na zilizobaki ni za wafanyabiashara.

Habari Kubwa