TRA yavifunga vituo 12 vya mafuta 

13Jan 2018
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
TRA yavifunga vituo 12 vya mafuta 

RUNGU la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Mkoa wa Kilimanjaro, limevishukia vituo 28 vya mafuta, huku 12 vikifungiwa baadhi ya pampu kutokana na kuendesha biashara bila ya kuwa na mashine za kielekroniki.

Vituo hivyo vinadaiwa kukiuka makubaliano ambayo yaliwataka wafanyabiashara wanaoviendesha wawe wamefunga mashine maalumu zenye uwezo wa kutoa stakabadhi za kielekroniki (EFD) kwa wateja ifikapo Desemba 31, mwaka jana.

Meneja wa TRA mkoani Kilimanjaro, Msafiri Mbibo, aliithibitishia Nipashe jana, juu ya kufungiwa kwa vituo hivyo.

“Hatuna lengo la kuwazuia wafanyabiashara kufanya biashara, jambo muhimu wanalotakiwa kufanya ni kufuata sheria, tuliwapa muda wa kutosha wa kufunga mashine hizo za kielekroniki, lakini hawakufanya hivyo,” alisema Mbibo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015 na kanuni zake za mwaka 2016, mfanyabiashara anayethibitika kukwepa kutumia au kutoa risiti za kielekroniki anaweza kukabiliwa na adhabu ya faini ya Sh. milioni tatu hadi milioni 4.5.

Aidha, sheria hiyo inaeleza mnunuzi anayekutwa na kosa la kutodai risiti, adhabu yake ni faini kati ya Sh. 30,000 hadi Sh. 150,000 au kifungo au adhabu zote kwa pamoja.

Hata hivyo, TRA Kilimanjaro inaonekana kubuni mbinu mpya ya kufanya kazi kwa kupiga kambi katika baa kubwa na klabu za usiku ambazo maarufu mjini Moshi, hatua ambayo inachukuliwa kuwakumbusha wafanyabiashara kutoa risiti za EFD.

     

Habari Kubwa