TRA yawaita wanaotaka vitambulisho vya machinga

13Jan 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
TRA yawaita wanaotaka vitambulisho vya machinga

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema mfanyabiashara ambaye alipatiwa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) ambaye anahitaji kupatiwa kitambulisho cha machinga , afike katika ofisi za taasisi hiyo ili kufanyiwa tathmini kama ana sifa za kupewa huduma hiyo.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, picha mtandao

Vitambulisho vya wajasiriamali wadogo vilizinduliwa na Rais John Magufuli na vimekuwa vikiuzwa kwa Sh. 20,000 kwa wenye mitaji ya chini ya Sh. milioni nne.

Baada ya kutolewa kwa vitambulisho hivyo, wako baadhi ya watu ambao walilalamika kuwa mitaji yao haijafika kiwango hicho alichokisema Rais lakini wameingizwa katika mfumo wa TRA.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alipokutana na wanafunzi wa Chuo cha Diplomasia kwa lengo la kuwapatia elimu katika masuala mbalimbali ya kodi.

Kayombo alisema kama kuna mfanyabiashara ambaye anajua mtaji wake haujafika kiwango hicho afike ofisini ili afanyiwe tathimini na wakigundua atapatiwa kitambulisho hicho.

“Huyu mtu asizungumzie pembeni, aje kwenye ofisi za TRA tutathimini biashara yake kama anastahili kuwa nje yawigo basi atatolewa na kama anastahili kuwemo  atatolewa tutaangalia mauzo yake na uhalisia wa biashara hakuna mwananchi ambaye anastahili kuonewa katika ulipaji wa kodi,” alisema.

Aidha, alisema kama kuna wafanyabiashara ambao wamekadiriwa mapato makubwa wawasilishe malalamiko yao ili yafanyiwe kazi.

Alisema lengo la kukusanya kodi haina maana wanataka kuwakomoa wananchi, hivyo ataona malalamiko yake hayajafanyiwa kazi atakwenda kwenye mahakama ya rufani ya kodi na kupatiwa haki.

Aidha, Kayombo alisema elimu aliyoitoa chuoni hapo itawasaidia katika kuwajenga uzalendo  katika ulipaji wa kodi.

“Pia tumewaelimisha wajue kodi yao wanapoitoa inakwenda kufanya nini na wajibu wa mwananchi baada ya kodi kukusanywa ni kudai haki yake kwamba kodi imefanya jambo gani. Anapoona kodi yake imefanya maendeleo inampa moyo wa kuendelea kulipa tena,” alisema.

Alisema zamani watu walikuwa wanakwepa kodi na kujineemesha jambo ambalo limechukuliwa hatua na kwa sasa vielelezo vinaonekana vya matumizi ya kodi.

Kayombo alisema wananchi wanapaswa kuwaripoti watu ambao wanakwepa kulipa kodi ili sheria ichukue mkondo wake ili wajisajili na kuanza kulipa kodi.

“Tunataka watoe risiti kwa usahihi unapotoa risiti kwa usahihi maana yake kodi itakusanywa kwa usahihi na wajibu wa mwananchi ni kudai risiti na sio kusubiria kupatiwa risiti,” alisema.

Naye  Kaimu Mkurugenzi wa Chuo Cha Diplomasia, Dk. Benard Achiula, alisema wameamua kuwaalika TRA chuoni hapo ili wawaelimishe wanachuo umuhimu wa kulipa kodi.

Alisema wameamua kumsaidia Rais Magufuli katika kuelimisha wananchi katika kulipa kodi, hivyo wananchi wanatakiwa kuunga mkono jitihada hizo ili kujenga uchumi kupitia mapato ya ndani na kujitegemea.

Habari Kubwa