TRA yawakumbusha wafanyabiashara matumizi sahihi ya EFD

23Oct 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
TRA yawakumbusha wafanyabiashara matumizi sahihi ya EFD

WAFANYABIASHARA wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya EFD ,ulipaji wa kodi wa hiari na utunzaji wa kumbukumbu ili kuwaewezesha maofisa wa TRA kukadiria kodi stahiki na kuepuka kukusanya kodi zisizo na msingi.

Hayo yamebainishwa na Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara jijini Mwanza kuhusu masuala mbalimbali ya kodi na matatizo yanayowakabili ili kwa pamoja wapate ufumbuzi  alieleza kuwa TRA inaendelea kuimarika na kuongeza bidii ya kufanya maboresho ya mfumo itakayorahisisha ukusanyaji kodi.

Amesema wafanyabiashara wote wahakikishe wanatumia mashine hizo kwa usahihi na kutoa risiti kwa kila mauzo na wananchi wanapaswa kudai risiti na atakayekiuka sheria itachukua mkondo wake kwa kutoa adhabu kali kwa kulipa fedha isiyopungua million 3 hadi milioni 4.5 kwa kitendo kimoja, kifungo au vyote kwa ujumla pia utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu katika ukadiriaji na ukusanyaji wa kodi.

Aidha, Kamishna Mkuu wa TRA anaeleza kuwa mchango wa wafanyabiashara wa ulipaji kodi ni chachu kuu ya maendeleo ya Taifa hivyo aliwasisitizia ulipaji wa hiari na watengeneze mipango ya kulipa madeni ya nyuma na TRA isingependa kurudi nyuma kwenye matumizi ya nguvu katika ukusanyaji.

Akizungumzia suala la kukamata na kutaifisha bidhaa na vyombo vilivyotumika kusafirisha magendo katika ukanda wa Ziwa Victoria Kamishna Mkuu Kidata, alieleza kuwa ni wakati wa wafanyabiashara kuacha biashara za magendo kwa kutumia mipaka isiyo kuwa rasmi .

"Biashara ya magendo ina athari nyingi mbali na kusababisha upotevu wa mapato ya serikali ina atarisha afya za walaji wa bidhaa husika pia idara ya ushuru na forodha imekuwa ikiendesha minada ya bidhaa zilizoingizwa nchini kinyume na utaratibu ambavyo idadi kubwa hukamatwa katika Kanda ya Ziwa Victoria hiyo inachangia na ukanda huu kuwa na mipaka rasmi na nchi jirani za Kenya na Uganda" ameeleza Kamishina Mkuu .

Naye Kamishina wa walipa kodi Wakubwa Alfred Mregi amesema kuwa yote waliyoyaeleza wafanyabiashara yatasaidia katika kuboresha na kuleta ufanisi mkubwa katika utendaji kazi na kuleta maendeleo kwa Taifa.

Nao wafanyabiashara waliohudhuria mkutano huo wameipongeza TRA kwa kuja kivingine kwa kukutana na wafanyabiashara ili kujadiliana na kutatua changamoto mbalimbali za kikodi.

"Umekuwa mkutano mzuri kwetu kama wafanyabiashara na tumepata muda wa kuwasilisha kero zetu kwa kwa Kamishna Mkuu wa TRA. Tuna Imani anaenda kuzishughulikia ili nasi tulipekodi kwa mujibu wa Sheria, "alielezase Mwanabure Ihuya, Makamu mwenyekiti Chemba ya wafanyabiashara wa Viwanda, Kilimo na Biashara (TCCIA).

Habari Kubwa