TRC yaendelea kutoa elimu kwa wananchi ujenzi SGR Mwanza -Isaka

11Jul 2021
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe Jumapili
TRC yaendelea kutoa elimu kwa wananchi ujenzi SGR Mwanza -Isaka

SHIRIKA la Reli Tanzania – TRC linaendelea na kampeni maalum ya utoaji wa elimu kwa jamii zinazoishi maeneo yatakayopitiwa na mradi juu ya ujenzi wa Reli ya kisasa SGR, awamu ya kwanza kipande cha tano, Mwanza – Isaka (Km 341).

Kampeni hiyo iliyozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Luhumbi, Juni 28,2021, ambapo kabla ya uzinduzi huo timu ya mawasiliano kutoka TRC walizungumza na viongozi kutoka Wilaya ya Kwimba, Misungwi na Nyamagana. 

Lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha uelewa sahihi wa masuala yanayohusiana na mradi kwa viongozi na wananchi kwa ujumla wanakuwa nao ili kufikia maendeleo.

“Mradi  huu ni shirikishi, kwahiyo tunafanya kampeni hii ili kuhakikisha mradi unakuwa na tija kwa wananchi ambao ndio walipa kodi zinazotumika katika utekelezaji huu.

Tunataka mradi ubadilishe maisha ya watu kwa kuwaletea maendeleo” alisema Meneja Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa SGR Kipande cha Mwanza – Isaka, Mhandisi Machibya Masanja, wakati akitoa ufafanuzi wa kampeni hiyo katika moja ya mikutano ya hadhara.

Kampeni hiyo mpaka sasa tayari imewafikia wananchi wa Kata za Malya, Mwandu na Mantale wilayani Kwimba na Ukiriguru, Mamaye na Kolomije  wilayani Misungwi.

Katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika kata hizo, wananchi walijitokeza kwa wingi ambapo pamoja na kupata maelezo ya kina kuhusu mradi  huo, wananchi hao wameeleza jinsi ambavyo wameipokea kampeni hiyo kuhusu mradi huo.

“Elimu hii itatusaidia sana hasa sisi vijana, maana fursa ni nyingi kutokana na mradi huu kwahiyo elimu hii iatatusaidia kuzitambua Zaidi, lakini pia tunaahidi kuulinda mradi” alisema Mathias Nyama, mkazi wa kijiji cha Kitunga, Kata ya Malya wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Luhumbi, aliwahakikishia wakazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa, kuwa wananchi wote watakaopitiwa na mradi huo, kipande cha Mwanza Isaka, watalipwa stahiki zao kwa mujibu wa sheria.

Aidha kampeni hiyo inategewa kuwafikia viongozi na wananchi wa Mkoa wa Simiyu na Shinyanga ambayo pia inapitiwa na kipande cha tano cha Ujenzi wa Reli ya Kisasa (Mwanza – Isaka) kinachogharimu kiasi cha Sh. Trilioni 3.0617 za Kitanzania.

Habari Kubwa