TTB: Olduvai Gorge ipo katika ardhi ya Tanzania

02Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe
TTB: Olduvai Gorge ipo katika ardhi ya Tanzania

BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imetoa ufafanuzi wa taarifa zinazosambazwa katika mitandao kuhusu eneo la Olduvai Gorge kuwapo nchini Kenya, ikisisitiza kuwa eneo hilo lipo Tanzania.

Historia ya binadamu inaanzia Tanzania.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na TTB jijini Dar es Salaam jana ilisema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikifuatilia video iliyotumwa katika YouTube https://www.youtube.com/watch?=iveX49WE7fw na imekuwa ikisambazwa kupitia njia mbalimbali za habari ikimuonyesha mtu mmoja kutoka nchi jirani akisema kuwa Olduvai Gorge ambayo kimsingi iko Tanzania, kwamba iko Kenya.

Ilisema kimsingi eneo hilo la Olduvai Gorge liko katika Bonde la Ufa katikati ya Bonde la Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Manyara nchini Tanzania.

Ilifafanua kuwa video hiyo imeibua majadiliano katika mitandao ya kijamii baina ya Watanzania na watu wengine ambao wanaitakia mema Tanzania na wanaoelewa vizuri kuwa Olduvai Gorge iko Tanzania.

Taarifa ilibainisha kuwa TTB kama taasisi ya umma yenye jukumu la kuvitangaza vivutio vya utalii, imeshtushwa na video hiyo iliyojaa upotoshwaji ambao wanaamini mbali ya malengo mengine, ililenga kuchafua kazi nzuri inayofanywa na TTB kwa kushirikiana na wadau wengine katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwamo Olduvai Gorge.

Ilieleza kuwa TTB inapinga vikali upotoshwaji huo uliofanywa na mtu huyo wakati akihutubia mkutano ambao ulikuwa ni wa Vijana wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Amerika Agosti, mwaka jana.

Aidha, taarifa ilifafanua kuwa TTB inapenda dunia ifahamu kuwa kama ilivyo kwa Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Zanzibar na nyinginezo, Olduvai Gorge mahali panapoaminika kuwa ndipo binadamu wa kwanza duniani aliishi na ambako Dk. Louis na Mary Leakey, waligundua fuvu la binadamu huyo wa kale anayesadikiwa kuishi miaka takriban milioni mbili iliyopita, iko pia Tanzania na si mahali pengine popote duniani.

"TTB inatoa wito kwa Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi zao za kuvitangaza vivutio vya utalii kwa kujibu na kusahihisha papo hapo upotoshaji kuhusu Tanzania unapotokea ndani ya nchi au nje," ilisema taarifa hiyo.

Habari Kubwa