TTCL yafanya mapinduzi kwenye bidhaa zake

09Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TTCL yafanya mapinduzi kwenye bidhaa zake

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), limezindua maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja huku likisisitiza kuleta mapinduzi makubwa kwenye utoaji huduma na ubunifu wa bidhaa zake.

Akizindua maadhimisho hayo jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Balozi mteule Mohamed Mtonga, alisema Shirika litaendelea kufanya mapinduzi makubwa eneo la utoaji huduma pamoja na ubunifu katika bidhaa zake ili kuhimili ushindani uliopo sokoni.

Alisema ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa mwaka unaoishia Desemba 2018, ilibaini kuwa TTCL ni Shirika la huduma za mawasiliano linalokua kwa kasi, huku likiongoza kwa idadi ya ongezeko la wateja na hata huduma ya T Pesa nayo ikitajwa miongoni mwa huduma zinazostawi kwa kasi kubwa.

"Hadi sasa, tumeweza kuwafikia asilimia mbili ya wateja wa huduma za simu nchini, yaani wateja zaidi ya milioni mbili huku huduma ya T Pesa ikifikisha wateja zaidi ya 400,000, mawakala 14,000 na miamala ya takribani Sh. bilioni tano," alisema.

Alisema katika kuwajali zaidi wateja wake kihuduma TTCL imezindua rasmi huduma ya TTCL 'App' na namba maalum ya 'WhatApp' ya huduma kwa wateja kuboresha zaidi huduma zake.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Waziri Kindamba, alisema wanawapatia wateja wao huduma mpya na mwaka huu itaenda sambamba na utoaji wa zawadi kemkem za kuonyesha shukrani kwa wateja wao.

"Mwaka huu 2019, tunawaletea huduma ya TTCL 'App' itakayowawezesha wateja wa TTCL kujiunga na vifurushi, kuongeza salio na kupata salio la akaunti yake kupitia simu za mkononi na 'tablets'."

Akifafanua zaidi huduma hizo, alisema ndani ya TTCL App mteja ataweza kuongeza na kuangalia salio kupitia App hiyo itakayopatikana bure kwa wateja wa TTCL bila kujali kama ana kifurushi cha intaneti muda huo.

"Wateja watakaotumia TTCL App watapata huduma za ziada kama dondoo za afya, soko la hisa na kubadilisha fedha, kuona matangazo mbalimbali ya TTCL, kuunga kifurushi kwa namba nyingine na kumnunulia rafiki muda wa maongezi.

"TTCL App haihitaji usajili maalumu ili kutumia. Sisi tumetimiza wajibu wetu, kazi kwenu wateja wetu, kufurahia huduma hii nzuri na rahisi sana kuitumia. Pamoja na TTCL App, tumewaongezea wateja wetu njia nyingine rahisi ya kuwasiliana nasi kupitia huduma ya WhatsApp na kwa namba 0738 151511, alisema.

Habari Kubwa