Tucta yaiita serikali mezani

06Dec 2018
Na Waandishi Wetu
MOROGORO
Nipashe
Tucta yaiita serikali mezani

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limewataka wafanyakazi kuwa watulivu wakati wanaendelea kuishauri serikali kufanya mabadiliko kwenye kikokotoo kipya cha malipo ya mkupuo ya asilimia 25 kwa wastaafu ili wafanyakazi waweze kunufaika na fedha zao.

Rais wa Tucta, Tumaini Nyamuhokya.

Shirikisho hilo limesema halikubaliani na kikokotoo kipya cha malipo ya mkupuo ya asilimia 25 kwa wastaafu na pensheni ya kila mwezi ya asilimia 75 itakayobaki kwa kuwa tangu mwanzo walipendekeza malipo ya mkupuo yawe asilimia 40 na asilimia 60 ibaki kwenye mfuko kama pensheni ya mwezi, lakini walishindwa kutokana na uamuzi kufanyika kwa kupiga kura.

Msimamo huo ulitangazwa jana na Rais wa Tucta, Tumaini Nyamuhokya, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa kamati ya utendaji ya Shirikisho hilo taifa, iliyokutana kwa siku mbili mjini hapa.

Alisema hoja ya kuweka usawa kwa wanachama wa mifuko, isingekuwa kupunguza asilimia 50 bali kuongeza waliokuwa wanalipwa asilimia 25 na miaka kuwa 15.5.

Kabla ya kanuni za mwaka 2018, NSSF na PPF walikuwa wanalipwa kwa kikokotoo cha asilimia 25, na PSPF, LAPF na GEPF, wakilipwa kwa asilimia 50.

Alisema Shirikisho hilo linaundwa na vyama 13 vya wafanyakazi na alikiri kwamba walishirikishwa vizuri kwenye mchakato wa kutunga sheria na baadaye kanuni zilipokuwa tayari walishirikishwa pia.

“Tucta tulishiriki vyema katika mchakato wa sheria na kutoa maoni na msimamo wetu kwenye vikao mbalimbali. Mapendekezo yetu kwenye sheria yalizingatiwa kwa kiwango kikubwa sana, tatizo limekuja kwenye utungwaji wa kanuni,” alibainisha.

Aidha, alisema hoja ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini ilianzishwa na wafanyakazi mwaka 2014, ikiwa na lengo la kuboresha mafao ya wafanyakazi na wastaafu.

“Wafanyakazi tuliamini kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ikiunganishwa gharama za uendeshaji na ushindani usiokuwa na tija kwa mfanyakazi ingepungua na mifuko kuokoa fedha nyingi ambazo zingeelekezwa katika uboreshaji wa mafao ya wafanyakazi,” alifafanua.

Nyamuhokya alisema, katika utungwaji wa kanuni hizo Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, ilishirikisha wadau wote wakiwamo Chama cha Waajiri Nchini (ATE), Tucta na Wataalamu toka mifuko ya hifadhi ya jamii.

Alisema kikao cha utatu kilifanyika Juni 7 na 8, mwaka huu na Ofisi ya Waziri Mkuu iliwasilisha kwa mara ya kwanza mapendekezo ya kanuni na walizipokea na kuomba muda wa kuzipitia.

Kwa mujibu wa rais huyo, Juni 12, mwaka huu, kikao kingine kilifanyika kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu na Tucta waliwasilisha maoni na mapendekezo ya kanuni hizo.

Mapendekezo yao

Alisema waliitaka serikali kuendelea na kanuni za mwaka 2017 zinazotoa malipo ya mkupuo kwa asilimia 50 na kikokotoo cha moja ya 540 na umri wa kuishi baada ya kustaafu uongezwe na kufikia miaka 15.5 badala ya 12 iliyowekwa sasa.

Alitoa mfano kwa mtumishi aliyestaafu baada ya kuchangia mfuko kwa miaka 30 akiwa amelipwa wastani wa mshahara wa Sh. milioni moja.

Nyamuhokya alisema kwa mapendekezo yao mtumishi huyo angelipwa pensheni nzima Sh. milioni nane, lakini kwa kikokotoo kipya atalipwa Sh. 7,448,276 ikiwa na tofauti ya Sh. 551,724.

Kwa malipo ya mkupuo kwa mapendekezo ya Tucta ni Sh. milioni 62 na kwa kikokotoo kipya ni Sh. 23,275,862 ikiwa ni tofauti ya Sh. 38,724,137.93.

Aidha, alisema hawakubaliani na hoja ya serikali kuwa kikokotoo kipya ni kunusuru mifuko ya PSPF na LAPF kufilisika na kwamba kufilisika kunatokana na uwapo wa deni kubwa la fedha ambazo serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kipindi kirefu.

“Tuliieleza serikali kuwa iwapo madeni yatalipwa ni wazi kuwa mifuko ingekuwa na uwezo wa kujiendesha, ikiwa ni pamoja na kulipa mafao ya wanachama kwa mujibu wa kanuni za mwaka 2017,” alisema.

“Tuliieleza serikali wafanyakazi hatukubali hoja ya mifuko kufilisika wakati tunafahamu kuwa mifuko imewekeza fedha nyingi za michango ya wanachama katika miradi na fedha nyingine zimetumika katika miradi mikubwa ya serikali kwa mikopo ambayo serikali inastahili kurejesha,” aliongeza:

“Haiwezekani serikali pamoja na menejimenti za mifuko zifanye makosa halafu mfanyakazi ndiye abebeshwe zigo kwa kupunjwa mafao yake ya pensheni ya kustaafu,” alisisitiza.

Walikata rufaa

Rais huyo alisema baada ya vikao zaidi ya vinane na kuishia kwenye kukubaliana kutokukubaliana, serikali ilishauri hoja za pande zote ziwasilishwe kwenye Baraza la utatu la ushauri (Lesco).

Alisema baraza hilo linaundwa na idadi ya wajumbe kwenye mabano Tucta (4), waajiri ATE (4) serikali (4) na wataalamu wawili chini ya wizara husika.

“Kwa mujibu wa sheria kikao cha Lesco ndicho kikao cha mwisho cha utatu kumshauri waziri katika masuala yanayohusu kazi ikiwa ni pamoja na utungwaji wa sheria na kanuni mbalimbali zinazowagusa wafanyakazi nchini,” alisema.

Kwa mujibu wa Nyamuhokya, kutokana na mvutano uliojitokeza ndani ya kikao cha Lesco kuhusu vikokotoo vya moja ya 580,  asilimia 25 na miaka 12.5 vilivyopendekezwa na serikali, wafanyakazi walipinga na kuamuliwa mwafaka kufikiwa kwa kupiga kura.

“Kutokana na uchache wa wawakilishi wa wafanyakzi ndani ya Lesco upande wa serikali na waajiri walishinda na waziri kuendelea na hatua za kutangaza kutumika kwa kanuni hizo,” alisema.

Alisema baada ya kikao hicho walikutana na waziri husika Julai 9, mwaka huu na kumweleza msimamo wao kuwa ni kikokotoo cha moja ya 580, miaka 15 na asilimia 40 na kumsihi kanuni hizo zisitangazwe.

“Waziri alitueleza kuwa wamelazimika kutangaza kanuni hizo kutokana na malalamiko ya muda mrefu kwa wastaafu wa mifuko iliyounganishwa na kutengeneza PSSSF ambayo yalisitishwa kusubiri ujio wa kanuni mpya,” aliongeza.

“Mfanyakazi kulipwa robo ya mafao yake na kubakiza robo tatu ni wazi kuwa wengi watakaopoteza maisha kabla ya kutimiza umri wa miaka 12.5 baada ya kustaafu fedha zake zitapotea wakati endapo angepewa kwa mkupuo zingemwezesha kuinua hali ya familia yake na jamii kwa ujumla,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa kanuni hiyo mpya, iwapo mstaafu atafariki kabla ya kutimiza miaka 12.5 ya kustaafu warithi wake watalipwa kwa miezi 36 tu ambayo ni miaka mitatu.

Rais huyo aliwataka wafanyakazi kuwa watulivu wakati wanaendelea kuishauri serikali kufanya mabadiliko kwenye kikokotoo hicho ili wafanyakazi waweze kunufaika na fedha zao.

 

Imeandikwa na Salome Kitomari na Ashton Balaigwa,

Habari Kubwa