TUCTA yawasilisha rasmi kwake kilio cha kikokotoo

02May 2022
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
TUCTA yawasilisha rasmi kwake kilio cha kikokotoo

SHIRIKISHO la Vyama Huru vya Wafanyakazi (TUCTA), limewasilisha mambo tisa kwa Rais Samia Suluhu Hassan ikiwamo kuongezwa kwa kiwango cha mkupuo wa pensheni(kikokotoo) kiwe kwa asilimia 33.

Akisoma risala ya wafanyakazi kwenye sherehe za Mei mosi mwaka 2022, Katibu Mkuu wa TUCTA, Henry Mkunda,alisema shirikisho hilo linafahamu mchakato wa upatikanaji wa kikokotoo bora cha mafao kwa wastaafu unaendelea na imekuwa ikishirikishwa na serikali kila hatua.

“Pamoja na kushirikishwa uandaaji wa kanuni mpya za mafao ya pensheni, tunapendekeza kuongezwa kiwango cha mkupuo wa kiwango cha pensheni kutoka asilimia 25 iliyokataliwa awali angalau ifikie asilimia 33, tumeomba pia serikali iridhie mapema mapendekezo ya kanuni iliyopendekezwa na kamati ya uongozi,”alisema.
 
Kuhusu kima cha chini cha mshahara kwa sekta zote za umma na binafsi, alisema wafanyakazi hawajaongezwa mishahara kwa takribani miaka tisa kwa sekta binafsi na miaka saba kwa sekta ya umma hali hiyo imesababisha kupungua kwa ari ya kufanya kazi hivyo kupunguza ufanisi na uwajibikaji na tija mahali pa kazi.

Mkunda alisema ni wazi gharama za maisha zimezidi kupanda na ilihali stahiki na ujira wa wafanyakazi umeendelea kuwa duni na kubainisha kuwa kwa sasa mshahara wa kima cha chini kwa sekta binafsi ni kati ya Sh.40,000 hadi Sh.60,000 kwa mfanyakazi wa majumbani.

Aidha, alisema kwa wafanyakazi wa mashambani na viwandani ni Sh.100,000 , viwango vilivyotangazwa mwaka 2013 katika gazeti la Serikali na kwa upande wa wafanyakazi wa umma, kima cha chini cha mishahara ni Sh. 300,000 kilichotangazwa mwaka 2015.

“Kufuatia hali hiyo,  TUCTA ilifanya utafiti mwaka 2006 na kuwasilisha mapendekezo serikalini mapendekezo kuwa kima cha chini cha mshahara kinachomwezesha mfanyakazi kumudu mahitaji muhimu kwa wakati huo Sh.315,000 ingetosha kumudu gharama za maisha.”

“TUCTA ilifanya utafiti mwingine mwaka 2014 na kubaini kuwa malipo ya mshahara ya Sh.720,000 kwa mwezi yangemwezesha mfanyakazi wa kima cha chini kumudu gharama za maisha,”alisema.

Alisema pamoja na mapendekezo hayo viwango hivyo havijakubaliwa na Serikali na kwamba kutokubaliwa kwa mapendekezo hayo kumeathiri wafanyakazi na familia zao kutokana kupanda kwa gharama za maisha na kuwafanya kuishi maisha ya chini ya mstari  wa umasikini.

Pia alisema bado wana kilio cha kodi kwenye marupurupu mengine na kuomba wakiangalia zaidi itasaidia kupunguza makali ya maisha.

Kuhusu Bima ya Afya, aliomba waangalie gharama za baadhi ya magonjwa makubwa na kuwawezesha sekta binafasi kupata huduma ya matibabu hata baada ya kustaafu.

Alilalamikia kitendo cha wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa mikataba kwa muda mrefu bila ya kupewa ajira.

Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, aliomba kasi ya kuwarejesha kazini watumishi waliokuwa na elimu ya darasa la saba ambao waliondolewa kazini lakini wamesoma na kuhitimu kidato cha nne iongezwe na wale ambao walikuwa wamefikia umri wa kustaafu wapewe mafao yao ili yawasaidie.

Aidha, aliomba bodi ya mishahara ya sekta binafsi ikae kwa haraka ili na watu wa sekta hiyo nao wapandishiwe kima cha chini cha mishahara.

Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Nchini (ATE), Jayne Nyimbo, alisema kuna mlundikano wa kodi zinazotozwa nchini ambazo zimeongeza gharama kwa waajiri.

Habari Kubwa