Tuhuma rushwa zawaweka matatani mwanajeshi, polisi

23Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Bukoba
Nipashe
Tuhuma rushwa zawaweka matatani mwanajeshi, polisi

MWANAJESHI na askari polisi ni miongoni mwa watu wanne waliotiwa mbaroni na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kagera, kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.

Mkuu wa Takukuru mkoani Kagera, John Joseph, picha mtandao

Taasisi hiyo imesema imewakamata watu hao wanne kwa tuhuma za makosa mbalimbali wilayani Biharamulo mkoani humo.

Mkuu wa Takukuru mkoani Kagera, John Joseph, aliwaambia wanahabari jana kuwa Oktoba 12, mwaka huu, walimkamata askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Koplo Nyambita Makayaga Magoma, ambaye ni mkufunzi ofisi ya Mgambo katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo.

Alisema akiwa katika Kijiji cha Nemba, askari huyo alikamata ng'ombe wa mkazi wa wilaya hiyo kwa madai ya kuwa wameingia katika msitu wa akibai na kuomba rushwa ya Sh. milioni 3 ili asimchukulie hatua za kisheria.

“Askari huyo aliomba Sh. milioni 3 kutoka kwa mwananchi huyo kwa madai kuwa ng'ombe wake wameingia katika hifadhi kinyume cha sheria,” alisema Joseph.

Aliongeza kuwa askari huyo alishikilia mifugo hiyo hadi alipopatiwa Sh. l,800,000 kisha kumwanchia mwananchi huyo.

Aidha, Takukuru inashikilia watu wengine wawili akiwamo askari polisi wa kituo cha Runazi, Koplo Nassor Maulid, kwa tuhuma za kushirikiana na ofisa misitu wa halmashauri hiyo kuomba rushwa ya Sh. 700,000.

Kwa mujibu wa Joseph, wawili hao waliomba fedha hizo kutoka kwa mfanyabiashara ya mkaa aliyekuwa amebeba magunia 50. Alisema Koplo Maulid alipokea fedha hizo kwa awamu mbili, ambapo ya kwanza alipokea Sh. 250,000 na kupokea tena Sh. 148,000 kabla ya kukamatwa.

Katika hatua nyingine, Joseph alisema kuwa ofisa wa halmashauri hiyo, Audax Norbert, anatuhumiwa kwa kuomba rushwa kutoka kwa mfanyabiashara ya bucha Sh. 200,000 ili asimfungie bucha baada ya kumkuta na makosa katika shughuli za ukaguzi.

Aliongeza kuwa mfanyabiashara huyo alimpatia ofisa huyo shilingi 50,000 kwa hofu ya kufungiwa bucha yake.

Joseph alieleza kuwa uchunguzi wa tuhuma hizo ukikamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.

Habari Kubwa