"Tuhuma za DC Sabaya si za kweli" - Kilimanjaro

24Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
KILIMANJARO
Nipashe
"Tuhuma za DC Sabaya si za kweli" - Kilimanjaro

JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limesema, hakuna hujuma wala uharibufu wa miundo mbinu ya Reli katika eneo la Kijiji cha Rundugai wilaya ya Hai, kama ilivyoelezwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salum Hamdun, amesema kuwa baada ya Mkuu wa wilaya Hai, Ole Sabaya kutoa tuhuma hizo na kuagiza wafanyabiashara wawili wa mabasi ya abiria, kujisalimisha polisi, walitii agizo hilo na baada ya kutoa maelezo waliachiwa kwa dhamana.

"Uchunguzi wa awali umebaini kuwa hakuna miundombinu ya Reli iliyoharibiwa au kuhujumiwa katika himaya hii kwa maana ya kipande cha kutoka Moshi kuelekea Arusha, ambapo mpaka sasa kimeshakarabatiwa kwa Kilomita 23 na kazi inaendelea" amesema RPC Kilimanjaro.

Ikumbukwe kuwa Januari 19, 2020, Mkuu wa Wilaya ya Hai  Lengai Ole Sabaya, akiwa katika kijiji cha Rundugai akikagua ukarabati wa Reli, alitoa agizo kwa wafanyabiashara wawili wa mabasi ya Lim Safari na Machame Safari ambao ni Rodrick Uronu na Clemence Mbowe, kujisalimisha katika kituo cha Polisi cha Bomang'ombe kwa tuhuma za kuunda genge la uhalifu ili kuathiri usafiri wa Treni ya abiria kati ya Dar es Salaam ,Moshi na Arusha.

Chanzo: Eatv

Habari Kubwa