Tulia atetea wabunge wa CCM kusema ‘ndiyo’

13Jan 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Tulia atetea wabunge wa CCM kusema ‘ndiyo’

NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, amesema wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wamekuwa wakisema ‘ndiyo’ katika kupitisha bajeti ya serikali kwa ajili ya fedha za miradi ya maendeleo, ndio wamewezesha kufanikisha mambo makubwa kufanyika nchini.

NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson picha mtandao

Dk. Tulia aliyasema hayo juzi mbele ya Rais John Magufuli katika hafla ya mapokezi ya ndege ya pili aina ya Aibus A220-300 iliyowasili jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, ikitokea Canada.

Alisema kumekuwa na kauli zinazowakebehi wabunge wa CCM kuwa wamekuwa wakisema ‘ndiyo’ kwa kila kitu bungeni dhana aliyodai ni tofauti kwa sababu ndio wanaochangia kukamilika kwa miradi ya maendeleo nchini.

“Nikueleze tu Mheshimiwa Rais, kumekuwa na kasumba kuwa wabunge wa CCM  wanasema ‘ndiyo’ bungeni. Wanaposema ‘ndiyo’ haya ndiyo matokeo yake. Wale wanaopinga hawataki haya yafanyike,” alisema Dk. Tulia.

Alisema wabunge wa upinzani ambao wamekuwa wakipinga bajeti za shughuli za miradi ya maendeleo, hawapendi kuona mafanikio hayo.

“Ningekuwa na muda ningetoa mifano mingi lakini haya yanayotekelezwa ni kwa sababu yalipitishwa na wabunge wa CCM,” alisema.

Alisema pia Rais Magufuli ametimiza ndoto za ajira kwa vijana waliokuwa na ndoto za kurusha ndege za Tanzania kutokana na kununuliwa kwa ndege hizo.