Tume ya madini kuvuka lengo ukusanyaji mapato

10Jul 2020
Dotto Lameck
Dar es Salaam
Nipashe
Tume ya madini kuvuka lengo ukusanyaji mapato

MTAKWIMU wa Tume ya Madini nchini, Azihar Kashakara, amesema Tume ya Madini imeweza kuvuka lengo walilopewa la kukusanya mapato ya Shilingi Bilioni 470 kwa mwaka 2019 – 2020 na kukusanya Shilingi Bilioni 528.2.

Kashakara amesema hayo katika banda la tume hiyo katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo jijini Dar es Salaam katika maonesho ya sabasaba, huku akisema kuwa tume hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika pato la serikali hadi nchi kufikia kwenye uchumi wa kati.

“Kupitia Tume ya Madini kuweza kukusanya kwa makini tozo mbalimbali zinazotokana na shughuli mbalimbali za madini zimeweza kusaidia kuwa na mchango mkubwa nchi kufikia uchumi wa kati” amesema Kashakara.

Kwa upande wake Meneja Habari na Mawasiliano wa Tume ya Madini, Greyson Mwase, amesema katika maonesho ya mwaka huu tume ya madini imeweza kushirikisha wachimbaji wadogo kama mfano wa kuwahamasisha wananchi ambao wanania ya kuingia kwenye uchimbaji mdogo wa madini.

“Maonesho yamekuwa na manufaa na tumejiandaa kikamilifu na tutaendelea kushiriki forum mbalimbali kwaajili ya kuhakikisha wawekezaji kutoka nje ya nchi wanakuja kuwekeza hapa nchini katika sekta ya madini na hasa ukizingatia nchi yetu tumeingia kwenye nchi yenye kipato cha kati na sisi tutaendelea kufana vizuri zaidi huku tukihakikisha sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa” amesema Mwase.

Habari Kubwa