Tume ya walimu yalia ukata

27Jan 2019
George Tarimo
IRINGA
Nipashe Jumapili
Tume ya walimu yalia ukata

TUME ya Utumishi wa Walimu (TSC) imesema ufinyu wa bajeti na vitendea kazi vimesababisha kufanya kazi katika mazingira magumu.

Katibu wa TSC, Winfrida Rutaindurwa, alisema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa baraza la wafanyakazi la tume hiyo, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, mjini hapa.

 

Alisema bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2018/19 haikidhi utekelezaji wa majukumu ya kisheria ya tume hiyo, hivyo kusababisha ishindwe kufanya kazi zake kama ilivyokuwa imedhamiria.

 

Rutahindurwa alisema mwaka wa fedha wa 2018/19 tume iliidhinishiwa zaidi ya Sh. bilioni 12.5 na kati hizo, Sh. bilioni saba zilitumika kulipa mishahara ya watumishi na Sh. bilioni nne zimetumika kwa ajili ya matumizi mengine (OC).

 

Alisema mkutano huo wa baraza wa siku mbili, umelenga kujadili mambo mengi ikiwamo muundo wa utumishi wa walimu na majukumu yake kama ilivyoidhinishwa na Rais John Magufuli Oktoba Mosi, mwaka jana, na kujadili mwelekeo wa bajeti ya tume kwa mwaka 2019/20.

 

Katibu huyo alisema ili tume itekeleze vyema majukumu yake vizuri, inaiomba serikali iwapatie nyongeza Sh. bilioni 8.6 katika bajeti yake.

 

Mkutano huo ni wa kwanza tangu kuanzishwa kwa baraza hilo mwaka 2016 ukiwa na lengo la kuongeza ufanisi katika kuwahudumia walimu ambao ni kundi kubwa linalochukuwa takribani asilimia 60 ya watumishi wa umma Tanzania Bara.

 

Akizungumza baada ya kuzindua baraza hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara, alisema serikali inatambua changamoto ya kifedha ambayo imewafanya wakwame kwa baadhi ya mambo, hivyo kuahidi ofisi yake kwa kushirikiana na walimu kuifanyia kazi.

 

“Kwa kuwa tume ni moja ya taasisi zilizo chini ya ofisi yangu, natambua kuwa changamoto hiyo ni kubwa na kwa sababu hiyo ofisi yangu itaendelea kushirikiana nanyi katika kutafuta ufumbuzi wake,” alisema Waitara.

 

Habari Kubwa