Tundu Lissu ajinadi mikoa mitatu

13Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Tundu Lissu ajinadi mikoa mitatu

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ameendelea kuchanja mbuga kwenye mikoa ya Singida, Tabora na Shinyanga huku akisema uchaguzi huu hautakuwa rahisi kwa kuwa kura ya mwaka huu ni ya ukombozi wa nchi.

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Akizungumza jana katika mikutano tofauti ya maeneo ya Iramba mkoani Singida, Igunga na Nzega Mjini mkoani Tabora na Kagongwa wilayani Kahama, alisema kuwa Watanzania wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kumpa ushindi ikiwamo kulinda kura.

Alisema kwa miaka mitano baadhi ya wananchi wamepitia changamoto mbalimbali ikiwamo za watu kujeruhiwa, kupoteza maisha, kujeruhiwa na wengine kuwa na kesi katika Mahakama mbalimbali nchini.

Alisema kura ya mwaka huu ni muhimu sana kwa kuwa ndiyo wakati wa ukombozi kwa Watanzania kuondokana na madhila mbalimbali, huku akitaja baadhi ya matukio ikiwamo la yeye kushambuliwa kwa risasi mwaka 2017.

“Chagueni mtu wa haki na atakayesimamia haki kwa maneno na vitendo na kwa maendeleo ya watu, ifikapo Oktoba 28, mkapige kura ili Oktoba 29, tuondokane na kero ya vitambulisho vya machinga,” alisema, huku akimtaka mmoja wa wananchi aliyenyanyua kitambulisho kujibu maswali.

“Naomba uwaambie wananchi wa Nzega kama hicho kitambulisho kina jina lako, waambie kama kina picha yako, waambie kama kimeeleza unapokaa au unapotokea, kama kina mwaka wa kuzaliwa na sahihi yako, umekinunua  20,000?” Alihoji.

Kwa mujibu wa Lissu, anataka kujenga nchi ya watu walio huru kukosoa na kuzungumza mawazo yao, na kutaka wananchi wanaochukizwa na hayo kupigakura kwa wingi.

“Tunahitaji kura hata ya CCM, kwa sababu tunahitaji kura ya kila mmoja, kama mtu anasikiliza mkutano na ni CCM mwacheni sababu tunahitaji kura zao,” alisema Lissu.

Alisema kura ya wananchi hao kwa chama hicho, Igunga, itawaondolea kero wanayoipata kutoka kwa Mmalaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kodi kubwa zinazowaumiza.

“Kwa mwaka huu uchaguzi hautakuwa rahisi, namna pekee ya kushinda ni kupiga kura, nchi nzima iimbe. Tukapige kura kwa ajili yetu, watoto wetu, wajukuu wetu sababu ni kura ya ukombozi, iwe kura ambayo itainua haki na haitatapanya mali,” alisema Lissu.

Aidha, Lissu alisema wasimamizi uchaguzi kwenye maeneo ya kupigia kura iwapo watakataa kuwaapisha mawakala wao, itakuwa ni kinyume cha kanuni za taratibu za uchaguzi.

“Mawakala kuingia kwenye vituo vya kupigia kura baada ya majina kuwasilishwa, msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri akipewa majina ni haki yao kuwapo hapo,” alisema.

Alisema askari Polisi watakaofuata kanuni na sheria hawapaswi kuwa na hofu katika utekelezaji wa majukumu yao, na kwamba serikali ya CHADEMA itawalinda ikiwamo kujali maslahi yao ambayo alidai hayajaboreshwa kwa miaka mitano.

Aidha, alilaani uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuwaengua wagombea wa CHADEMA kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kuzuiliwa kufanya kampeni na matukio ya kupigwa na kuuawa kwa baadhi ya wafuasi wa chama hicho bila hatua kuchukuliwa kwa haraka.

Habari Kubwa