Tundu Lissu kusaka wadhamini Kaskazini

13Aug 2020
Woinde Shizza
Arusha
Nipashe
Tundu Lissu kusaka wadhamini Kaskazini

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, na mgombea mwenza wake, Salim Mwalimu, wanatarajia kutua Arusha kesho kwa ajili ya kusaka wadhamini katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, alibainisha hayo alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za kanda za chama hicho.

Alisema wanatarajia kuwapokea Lissu na Mwalimu kwenye Uwanja wa Ndege wa Arusha na baadaye watakuwa na mikutano mifupi jijini.

Lema aliwataka wanachama wa CHADEMA kujitokeza kwa wingi kuwapokea wagombea wao hao kwa kuwa ngome kuu ya chama hicho ni Kanda ya Kaskazini.

"Baada ya kumpokea, tutakuja naye hapa, wanachama pamoja na viongozi wa chama waliojitokeza kumleta mpaka ofisini na kufanya mkutano mfupi kwa ajili ya kumdhamini na hotuba fupi itakuwapo.

"Likiisha hilo, mgombea wetu ataondoka na kuelekea katika maeneo mengine na kila eneo tayari ratiba zimeshatolewa na maelekezo ya kiofisi tayari, kinachotakiwa ni tujiandae tu kwa ugeni huo.

"Niwaombe tu wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kumdhamini mgombea na safari hii sisi kama CHADEMA tumejipanga kupeleka zaidi ya idadi ya wadhamini ambao tume wamependekeza," alisema Lema.

Kiongozi huyo wa kanda pia alisema uchukuaji wa fomu za kuomba kuwania nafasi za ubunge na udiwani ulianza jana na baadhi ya wanachama wameshachukua.

Lema alisema kuwa yeye hatachukua fomu wiki hii na atangaza rasmi siku ambayo atachukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania tena ubunge wa Arusha Mjini.

"Tunaendelea kuangalia jinsi uchukuaji wa fomu unavyoenda na tuna watu kila upande wanafuatilia suala hili. Tunafuatilia kila mahali na niseme tu kwamba hatutakubali matendo maovu yaliyofanywa kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa yajirudie kipindi hiki," alisema.

Lema alitamba kuwa CHADEMA imetoa elimu kwa wagombea wake kufanya siasa za amani huku akiahidi kuwa hawatafanya fujo yoyote na watafuata sheria zote za uchaguzi zilizoelekezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Habari Kubwa