Tundu Lissu: Nikiwa Rais nitakubali kukoselewa

18Oct 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Tundu Lissu: Nikiwa Rais nitakubali kukoselewa

MGOMBEA Urais, Tundu Lissu (CHADEMA), amesema akichaguliwa kuongoza nchi, atakuwa tayari kukosolewa na wananchi.

Amesema kuna haja wananchi kutumia siku 10 zilizobaki kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, kujipanga kuchagua rais atakayewapa uhuru wa kumkosoa.

Lissu aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wilayani Manyoni mkoani Singida katika mkutano wake wa kampeni.

Akihutubia wananchi hao, mgombea huyo alisema: “Mkapige kura mpate uhuru wa kuwasema hao mnaowapa uongozi. Wakikosea, wasemwe, wakifanya makosa ya kihalifu, washughulikiwe, mkapige kura za haki."

Lissu alisema akipewa ridhaa hiyo, atatengeneza serikali itakayoangalia shida za wananchi kuwa kuwa hiyo ndiyo maana ya maendeleo ya watu.

“Ninawaomba wananchi wa Manyoni muwapigie kura madiwani wote 18 wanaogombea nafasi hii kwa tiketi cha CHADEMA, tukishinda 10 tunaunda Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni,” alisema.

Mtaalamu huyo wa sheria alidai wananchi wakiwachagua wabunge wa chama tawala, wakiingia bungeni huingiwa na hofu ya kuisema serikali.

Aliahidi kwenye mkutano huo kuwa akiwa Rais, atahakikisha Bunge linakuwa huru.

Mgombea huyo akiwa mkoani Tabora, alizungumzia kilimo cha tumbaku akisema badala ya kutoa neema kwa wananchi, kimekuwa kilio.

“Ili tutatue tatizo hili la bei ya tumbaku ambayo kwa sasa Tabora bei ya soko kwa kilo ni Sh. 200, tutashughulikia tatizo la kodi, tuwapunguzie kodi wanaonunua tumbaku kwenye viwanda.

“Tukiwapunguzia, hawatakuwa na mzigo mkubwa, tutawaambia wakanunue tumbaku kwa bei ya faida kwa mkulima,” alisema.

Lissu alisema wasipofanya hivyo, zipo nchi zinazolima zao hilo na kuzitaja baadhi kuwa ni Malawi na Zimbabwe ambazo alidai kwa sasa zinauza zaidi tumbaku.

"Watakimbia hapa na kwenda kwenye hizo nchi nyingine, wakikimbia na viwanda vyao watakimbia na ajira za vijana wetu, CHADEMA itashughulikia matatizo ya mfumo wa kodi,” alisema.

Lissu alisema CHADEMA itaweka utaratibu wa kulipa ruzuku kwenye mazao badala ya kupeleka fedha za serikali katika pembejeo peke yake.

Alisema agano lao na wakulima nchini ni kupunguza mzigo wa kodi wa wanunuzi ili kuwezesha bei ya mazao kama tumbaku kupanda.

Habari Kubwa