Tundu Lissu: Nitakuwa Rais wa katiba mpya

16Oct 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tundu Lissu: Nitakuwa Rais wa katiba mpya

MGOMBEA Urais (CHADEMA), Tundu Lissu, amewaomba wananchi wa Kanda ya Ziwa kumchagua katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu, akiahidi kuiongoza nchi kwa kufuata katiba mpya itakayopatikana.

Amesema nchi inahitaji katiba hiyo kwa sasa, ili kurudisha mamlaka kwa wananchi kujichagulia viongozi kwenye maeneo yao na kuwawajibisha wanapokosea.

Lissu aliyasema hayo jana akiwa katika mikutano ya kampeni wilayani Rorya mkoani Mara na Busega mkoani Simiyu.

“Ninataka niweke wazi, mimi nikuwa rais aina ya Nyerere. Kwanini? Kwa sababu Mwalimu Nyerere mwaka 1978 alikuwa anahojiwa na BBC kuhusu mamlaka yake, alisema hivi; 'kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi, mimi ninaweza kuwa na mamlaka ya kuwa dikteta’.

"Mimi nitakuwa rais wa katiba mpya. Nchi hii inahitaji katiba mpya na katiba mpya ni mkataba wa wananchi, kurudisha mamlaka ya wananchi,” alisema.

Lissu alisema katiba hiyo itarudisha mamlaka kwa wananchi kwa kuwawezesha kuchagua viongozi wao, wakiwamo wakurugenzi wa miji, majiji, wakuu wa mikoa na wilaya.

Katika mikutano yake hiyo ya kampeni, Lissu pia aliwaombea kura madiwani na wabunge wa majimbo katika kanda hiyo, akiwamo Ezekiah Wenje anayegombea ubunge wa Rorya.

“Hapa tupate mtu jasiri katika eneo la Rorya, kura ya pili mumpe Ezekiah Wenje, kura yako wa tatu ninaomba mnipigie niwe rais wa nchi hii. Tuchague madiwani, kazi ya diwani na mbunge ni kukutetea wewe na siyo kuitumikia serikali,” alisema.

Lissu alisema mfumo wa kodi hautakuwa wa kukusanya kodi kwenye maeneo yao na kuzipeleka hazina, badala yake zitabaki maeneo zinakokusanywa.

“Rais ndiyo kila kitu, ni katiba hii imempa mamlaka yote, tunahitaji katiba mpya ndugu zangu, nitakuwa rais atakayeleta katiba mpya, muundo mpya wa utawala, nitakuwa rais na mfariji mkuu," alitamba.

Lissu pia alisema akipata urais, atabadili mfumo wa elimu ili kuwa na mfumo utaojenga maarifa kwa wananchi ili waajirike katika soko la ndani na nje ya nchi.

“Watoto wetu watapata ujuzi, tutafumua mfumo wa elimu, siyo tu watapata elimu bora, bali tutafungua mipaka ili waende nchi zingine za wenzetu, hata ukitaka kwenda Afrika Kusini, nenda,” alisema.

Kuhusu sekta ya afya, Lissu alisema serikali yake itahakikisha kila Mtanzania anajiunga na mfumo wa matibabu kwa kutumia bima ya afya, ili kuwapunguzia gharama za matibabu wananchi.

"Ukienda hospitali sasa kabla hujatibiwa unalipia, wanaougua wakiwa na bima, wakienda hospitali hakuna haja ya kulipa pesa." alisema.

Alisema wananchi wakishaichagua CHADEMA, watakuwa na uhakika wa kupata uhuru na haki ya kulima, kuuza mazao na kuvua samaki bila bugudha.

*Imeandikwa na Christina Mwakangale na Frank Maxmillian (TUDARCo)

Habari Kubwa