Tutumie mwezi Mtukufu kumuomba M/Mungu aibariki Tanzania - Majaliwa

02May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Tutumie mwezi Mtukufu kumuomba M/Mungu aibariki Tanzania - Majaliwa

​​​​​​​WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewasisiza waislam wote nchini watumie Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan kwa kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki Tanzania, viongozi na wananchi wake wadumishe amani na mshikamano.

Ameyasema hayo leo Jumapili, Mei 2, 2021 katika Fainali za Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Qur’an yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yahusisha washiriki 15 kutoka nchi 11.

Pia, Waziri Mkuu ametoa rai kwa waumini wa dini ya kiislam nchini waendelee kuyaishi mafundisho wanayoyapata katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwenye maisha yao ya kila siku.

“Natambua mchango mkubwa wa waumini katika kuienzi na kuitunza amani kwa kufuata miongozo ya viongozi wetu kupitia mafundisho ya Qur’an ambayo hututaka kuepuka kuivuruga amani.”

“Mwitikio mkubwa tunaouona kwenye mashindano haya ni kielelezo cha amani, umoja na mshikamano tulionao.” Amesema Waziri Mkuu.

Aidha,  Waziri Mkuu amesema ni vema vijana hao waliohifadhi Qur’an wakaendelezwa kitaaluma katika fani zingine za elimu kwani uwepo wao ni muhimu katika kujenga jamii bora na yenye uadilifu.

Habari Kubwa