TV ya mtandaoni yawaponza

07Mar 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
TV ya mtandaoni yawaponza

MAHAKAMA ya Hakimu Kisutu imewahukumu watu wawili kulipa faini ya Sh. milioni 10 au kwenda jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kutuma maudhui kwenye mtandao bila leseni ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA).

Washtakiwa hao ni Emmanuel Sisala (32) na mfanyabiashara Juhudi Motda (39) na hukumu dhidi yao ilisomwa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustina Mmbando.

Wakili wa Serikali, Adolf Lema, alidai kuwa kati ya Januari 2018 na Februari 2020, katika Jiji la Dar es Salaam, kupitia televisheni mtandaoni ijulikanayo Jumo Television, walituma maudhui bila leseni ya TCRA.

Washtakiwa walikiri makosa yao na Upande wa Jamhuri uliomba mahakama kutaifisha mitambo na mali mbalimbali ikiwamo simu za mkononi, kamera na kompyuta.

Hakimu Mmbando alisema kwa kuwa washtakiwa wamekiri makosa yao, mahakama yake inawatia hatiani.

Alisema washtakiwa watalipa faini ya Sh. milioni tano kila mmoja na wakishindwa, watakwenda jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja.

"Mahakama hii inaamuru kutaifishwa vielelezo walivyokutwa navyo zikiwamo simu za mkononi kompyuta na kamera," alisema.
Washtakiwa hao walifanikiwa kulipa faini na kuachwa huru na mahakama.

Habari Kubwa