Uamuzi kesi ndogo ya Mbowe kesho

19Oct 2021
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Uamuzi kesi ndogo ya Mbowe kesho

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi inatarajia kutoa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ya ugaidi inayomkabili, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu kesho.

Mahakama itatoa uamuzi kama mshtakiwa wa pili Adam Kasekwa aliteswa kabla na wakati akitoa maelezo ya onyo na kama maelezo hayo yalichukuliwa ndani ya saa nne ama la.

Uamuzi huo ulitarajiwa kutolewa leo lakini yametokea mabadiliko kwa sababu ni siku ya mapumziko na sasa utatolewa kesho, hatua hiyo imefikiwa baada ya Mahakama hiyo mbele ya Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani kumaliza kusikiliza ushahidi wa mashahidi watatu kwa upande wa Jamhuri na watatu kwa upande wa utetezi.

Septemba 10, mwaka huu, Mbowe, Kasekwa, Mohammed Ling'wenya na Halfani Bwire, walisomewa mashtaka na walikana kula njama kufanya ugaidi ikiwamo kumsababishia majeraha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Shahidi wa kwanza katika kesi ya msingi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Kamishna wa Polisi Msaidizi, Ramadhan Kingai alitoa ushahidi na katika ushahidi wake alidai kumsikia Luteni Denis Urio, akisema mbele ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz kwamba kuna kundi la kihalifu linaandaliwa na Freeman Mbowe na wanataka kufanya vitendo vya kigaidi.

ACP Kingai alipotaka kutoa maelezo ya onyo ya Kasekwa kama kielelezo, Wakili Peter Kibatala alipinga kupokelewa kwa madai mteja wao aliteswa kabla na wakati wa kuchukuliwa maelezo hayo na kwamba yalichukuliwa zaidi ya saa nne.

Upande wa utetezi uliomba iwapo kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, mahakama ilikubali na mashahidi watatu upande wa mashtaka walitoa ushahidi wakionyesha kwamba mshtakiwa Kasekwa hakuteswa.

Mashahidi hao alikuwa ACP, Kingai, Inspekta Mahita Omari na Koplo Msemwa.

Upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi watatu ambao katika ushahidi wao walionyesha mshtakiwa Kasekwa aliteswa baada ya kukamatwa Moshi Agosti 5, mwaka 2020, alipofikishwa Kituo cha Polisi Moshi na alipofika Dar es Salaam Agosti 7, 2020 hakupigwa, lakini alipewa maneno yaliyomtia hofu akiwa Kituo cha Polisi Mbweni.

Mashahidi wa utetezi alikuwa Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na mke wa Kasekwa, lilian Kibona.

Mawakili wanaomtetea Mbowe ni Kibatala, Michael Mwangasa, Michael Rugina, Alex Masaba, Gaston Garubimbi, Deogratias Mahinyila, Hadija Aron, Selemani Matauka, Ferdnand Makole, Evaresta Kisanga, Marie Mushi na Jonathan Mndeme.

Mshtakiwa wa kwanza Halfani Bwire anawakilishwa na Wakili Nashon Nkungu na Jeremiah Mtobesya, mshtakiwa wa pili Adamu Kasekwa anawakilishwa na John Mallya na mshtakiwa wa tatu anawakilishwa na Dickson Matata.

Upande wa Jamhuri unawakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, Nassoro Katuga, Ignas Mwinuka, Esther Martin, Pius Hillar, Jenitreza Kitali, Abdallah Chavula na Wakili wa Serikali Tilimanyo Magige.

Habari Kubwa