Uazimaji ‘mawigi’ washamiri, daktari bingwa ataja madhara 

27Jun 2022
Jenifer Gilla
DAR ES SALAAM
Nipashe
Uazimaji ‘mawigi’ washamiri, daktari bingwa ataja madhara 

NI dhamira ya kila mwanamke kuwa na mwonekano mzuri anapokuwa sehemu yoyote yenye watu tofauti iwe ofisini, kwenye biashara au sherehe mbalimbali.

Moja ya kivutio kikubwa cha mwanamke ni kuwa na nywele nzuri, ziwe zimesukwa, kubanwa au kubandika nywele za bandia (wig) ili kuongeza mwonekano mzuri. 

Hata hivyo, ili kutimiza haja hiyo kunahitaji kipato cha kutosha kuhakikisha mhitaji anapata vitu muhimu ili mwonekano uwe kama alioudhamiria kwa siku hiyo, watoto wa mjini wanaita “kudamshi”.

Wengine hushindwa kumudu gharama za kununua na kutafuta njia rahisi ya kuazima kwenye saluni zinazotoa huduma hiyo.

Baadhi ya saluni zinazopamba wanawake wanaokwenda kwenye sherehe, zimetumia fursa hiyo kukodisha nywele za bandia (mawigi), kwa wanaoshindwa kununua kutokana na kuuzwa kwa gharama kubwa madukani.

Nipashe, ilitembelea baadhi ya saluni za kike zinazotoa huduma hiyo na kuwahoji wafanyakazi na wamiliki wa maduka hayo, akiwamo Mwajabu Salehe, mmiliki wa saluni Tabata, jijini Dar es Salaam, ambaye alisema hufanya biashara ya kuazimisha mawigi ambayo amedumu kwenye kazi hiyo kwa miaka saba na kumsaidia kuongeza kipato chake.

“Huwa ninakodisha kwa siku Sh. 5,000, baada ya saa 24 mtu anatakiwa alirudishe, na siku tatu hadi nne nafanya Sh. 10,000. Kwa wiki naweza kukodisha watu watano hadi 10 kutegemeana na msimu,” alisema.

Kwa mujibu wa Mwajabu kwa siku za kawaida anapata faida wastani wa Sh. 70,000 kwa wiki na biashara ikichanganya siku za mwisho wa wiki ambazo watu hutoka kwenye starehe na sherehe mbalimbali hupata Sh. 120,000 hadi Sh. 150,000.

“Kipindi cha kukaribia mwezi wa Ramadhani ndiyo napata wateja wengi wa kuwakodisha kwa sababu ndoa nyingi za Kiislamu hufungwa ambapo kwa siku anaweza kuazimisha mawigi matano na kujipatia Sh. 25,000, lakini msimu wa sikukuu kama Iddi, Krismasi na Mwaka Mpya,” alisema.

Naye Hadija Hiza, mfanyabiashara hiyo eneo la Vingunguti, alisema kinachowapa nguvu ya kufanya biashara hiyo ni uhitaji mkubwa wa nywele hizo kadri siku zinavyokwenda kutokana na bidhaa hiyo kuuzwa bei ghali.

“Mawigi wanayoyapenda wengi yanauzwa bei ghali madukani kuanzia Sh. 70,000 hadi 300,000, unakuta wakazi wengi wa Vingunguti uwezo wa kuyanunua hawana, kwa hiyo wakija hapa kwa ajili ya kujipamba tunawakodisha kama hivi, Sh. 5,000 kwa siku mtu akimaliza jambo lake anarudisha,” alisema.

UAMINIFU KWA MTEJAKuhusu uaminifu, Mwajuma alisema mawigi yake hayapotei kwa sababu anaowakodisha ni watu anaowafahamu ni rahisi kuwafuatilia anapoona siku za kurudisha zimezidi na faini ya kuchelewesha ni Sh. 5,000 kwa kila siku itakayozidi.

Theresia Charles (25), mmoja wa wanaokodisha bidhaa hiyo eneo la Vingunguti, anasema huduma ya kukodi mawingi inawasaidia kutimiza haja yao ya kupendeza bila  kutumia gharama kubwa.

“Inatusaidia sana sisi wenye kipato cha chini maana laki moja ya kununua wig sina, lakini nikija hapa napata kwa Sh. 5,000 kwa siku kama shughuli ni ya siku tatu au nne nalipia Sh. 10,000 ambayo naitoa mara moja au mbili kwa mwezi,” alisema.

UTUNZAJIAshura Athumani, mmliki wa saluni Tabata Segerea, alisema baada ya wateja kurudishi bidhaa wakishaitumia, huyaosha kwa sabuni ya kuoshea nywele na kukausha kwenye mashine ya kukaushia nywele kabla ya kumpa mteja mwingine.

Hata hivyo, alisema kitendo cha kuyaosha mara kwa mara husababisha kuharibika mapema hali iliyomkatisha tamaa ya kuendelea na biashara hiyo.

“Mimi nilikuwa nakodisha ila sasa nimeacha kwa sababu yamekuwa yakiharibika kutokana na kuyaosha mara kwa mara, wakati mwingine unamkodisha mteja anakwenda kubandika kwenye saluni nyingine anatia gundi nyingi kwa hiyo inabidi utumie nguvu kuitoa nayo inachangia kuharibu,” alisema.

USALAMA KIAFYA Daktari Bingwa wa magonjwa ya ngozi kutoka Hospitali ya Lugalo, Dk. Msafiri Kombo, alisema kitendo hicho kina madhara kiafya kwa kuwa kinasababisha magonjwa ya ngozi na kuambukizana ikiwamo mba na fangasi na wadudu kama chawa.

“Hatari ya kuvaa wigi lililovaliwa na mtu mwingine ipo sehemu mbili, hapo mtu anaweza kupata maambukizi ya fangasi au wadudu wanaopenda kukaa kwenye nywele ikiwamo chawa kama litakuwa halijasafishwa na vifaa vinavyoangamiza vimelea vyake,” alitahadharisha Dk. Kombo.

Alishauri wanawake wanaopenda urembo huo kuacha kuvaa vitu vilivyovaliwa na watu wengine ikiwamo nguo na mawigi ili kujiepusha na magonjwa ya ngozi yanayoambukizwa.

“Kikubwa wajitahidi wanunue yao wenyewe, kuazimana nguo, viatu na mawigi haishauriwi kiafya, ni muhimu kila mmoja hasa wanawake kuwa makini na vitu kama hivyo kwa sababu wanapoambukizwa wao ni rahisi kuambukiza watu walio ndani ya familia ikiwamo watoto ambao wanakuwa nao kwa ukaribu,” alisema.

Habari Kubwa