Ubakaji watoto watisha

17Jun 2019
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Ubakaji watoto watisha

WAKATI Tanzania ikiungana na mataifa mengine barani Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, takwimu zinaonyesha matukio ya ubakaji kwa watoto yanashika kasi nchini.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mipango na Uratibu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yokobety Malisa, akisoma moja ya mabango ya wanafunzi jana, kabla ya kuhutubia katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwenye viwanja wa Shule ya Msingi Makuburi wilayani Kinondoni, jana. PICHA: SABATO KASIKA

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo kwa mwaka 2018 watoto 2,365 walibakwa, idadi ambayo ni sawa na watoto 394 kwa siku.

Aidha, ripoti ya hali ya uhalifu kwa mwaka 2017 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya

Takwimu (NBS), inaonyesha katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2017, matukio ya

uhalifu dhidi ya watoto yalikuwa 13,457.

Kadhalika, kwa mwaka 2016 matukio hayo yalikuwa 10,551, na kwamba kati ya hayo, matukio ya ubakaji yalikuwa 2,984.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (Unicef), inaonyesha kuwa wabakaji wengi ni ndugu wa

karibu ambao wanaishi ndani ya familia.

Kutokana na hali hiyo Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimeiomba serikali na wadau wengine wa masuala ya haki za watoto kuendelea kupaza sauti zao ili kuhakikisha ukatili huo unapungua na ikiwezekana kumalizika kabisa.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben, ilisema kuwa matukio ya ubakaji wa watoto ni tishio kwa usalama wao, ukuaji wao kwa ujumla na maendeleo endelevu ya taifa.

"Mtoto ni taifa la kesho, endapo atafanyiwa ukatili leo, je, kesho taifa hili litaongozwa na nani? Tamwa tunasisitiza hatua kali za kisheria na mabadiliko mengine ya kisera ili

kumlinda mtoto dhidi ya ukatili," alisema Rose.

Aliwasihi wazazi, walezi kulipa uzito mkubwa suala la ulinzi kwa mtoto ili kuepusha ubakaji.

“Kupinga unyanyasaji, ubakaji na ulawiti wa watoto ni jukumu la jamii nzima na wakati umefika sasa kila mmoja kwenye nafasi yake awalinde watoto kwa kuripoti vitendo vya unyanyasaji vilivyofichika kwenye jamii yetu," alisisitiza.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika kila Juni 16, na kaulimbiu ya mwaka huu ni: "Mtoto ni msingi wa taifa endelevu, tumtunze, tumlinde na kumwendeleza."

Kwa upande wa Tanzania Visiwani, vitendo hivyo vimedaiwa kuongezeka licha ya Tanzania kuwa ni nchi iliyosaini na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda yenye lengo la kuwalinda watoto dhidi ya udhalilishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Mkurugenzi wa Miradi ya SOS Zanzibar, Asha Salim Ali, alisema licha ya serikali kuwa na sheria mbalimbali, sera na mipango ya kuwalinda watoto dhidi ya aina zote za udhalilishaji, bado vitendo hivyo vinaendelea kutokea ikiwamo kubakwa na kulawitiwa.

Alisema vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa watoto vinaripotiwa katika maeneo mbalimbali na kurudisha nyuma maendeleo ya watoto na kuminya uhuru wao.

Aidha, alisema licha ya Zanzibar kutekeleza mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, bado inakabiliwa na kiwango cha juu cha udhalilishaji ikiwamo utelekezwaji wa familia, ndoa za utotoni, ukatili wa kingono, na wa kimwili pamoja na watoto kubakwa na kulawitiwa.

Alieleza kuwa ushirikishwaji wa watoto ni moja kati ya haki za msingi za watoto na kwamba matumaini yake ni kuwa maadhimisho hayo yatawapa watoto fursa ya kucheza na kufarahi na kujifunza mambo mengi muhimu.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Huduma za Simu kwa Mtoto Zanzibar, Fatma Ahmada, alisema lengo kuu la maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni kuwakumbusha viongozi wa serikali na jamii kwamba maendeleo ya taifa hayawezi kupiga hatua bila ya kuwasaidia watoto katika kupata mahitaji yao muhimu.

Alisema bado kuna kundi kubwa la watoto wanaohitaji msaada ikiwamo watoto maskini na wenye mahitaji maalum.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akiwa mjini Geita, amewataka wakuu wa mikoa ambayo haijaanzisha mabaraza ya watoto kuanzisha haraka pamoja na madawati ya ulinzi wa mtoto shuleni.

Akiwa katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, kimkoa mkoani Geita jana, alitaka kila mkoa uhakikishe unaanzisha haraka mabaraza ya watoto pamoja na madawati ya kulinda watoto shuleni, ili kuhakikisha matukio ya ukatili wa watoto yanatokomezwa kabisa.

Alisema lengo kuu la maadhimisho hayo kila mwaka ni kutafakari hatua ambayo imefikiwa katika kupinga ukatili wa watoto na kulinda haki za watoto.

Alisema takwimu za utafiti wa afya za mwaka 2015/2016 zinaonyesha kuwapo kwa ongezeko la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hapa nchini hususani wasichana kiwango cha kitaifa, ndoa za utotoni asilimia 37, mimba za utotoni asilmia 27 na ukeketaji wasichana asilimia 10.

Aidha, alisema takwimu za Jeshi la Polisi za mwaka 2018 zinaonyesha kuwapo kwa matukio 14,419 ya ukatili yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi nchini ikilinganishwa na matukio 13,457 kwa mwaka 2017 ambalo ni sawa na ongezeko la matukio 1,034, asilimia 7.7.

Pia ameongeza kuwa mikoa mitano inayongoza kwa matukio ya ukatili nchini ni Tanga (1,039), Mbeya (1,001), Mwanza (809), Arusha (792), Tabora (616) na kwamba matukio yanayoongoza ni ubakaji, ulawiti pamoja na kusema kuwa takwimu hizo zinaonyesha kuwa mapambano bado yapo katika kutetea haki za watoto.

Naibu Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Plan International, Benatus Sambili, alisema shirika hilo linajishughulisha na utetezi wa haki za watoto ambalo linafanyakazi katika mikoa 13 nchini katika kuhakikisha ustawi na upatikanaji wa haki za msingi za watoto hasa wa kike tangu mwaka 1991 katika maeneo ya elimu, afya ya uzazi wa mama na mtoto pamoja na usafi wa mazingira, uwezeshaji vijana kiuchumi.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel Luhumbi, amesema kuwa viongozi pamoja na jamii wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wanalindwa na kusimamia haki zao na hivyo kuitaka jamii kutowatenga watoto wa kike kwa kuwa wote wana haki kupata elimu.

*Imeandaliwa na Salome Kitomari, Dar es Salaam, Rahma Suleiman, Zanzibar na Alphonce Kabilondo, Geita

Habari Kubwa