Ubalozi Marekani yapongeza tuzo Jamii Forum

18Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ubalozi Marekani yapongeza tuzo Jamii Forum

UBALOZI wa Marekani nchini umempongeza mmiliki wa mtandao wa Jamii Forum, Maxence Melo, kwa kutangazwa mmoja wa washindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa mwaka 2019. Tuzo inayotolewa na Kamati ya Ulinzi kwa waandishi wa habari.

UBALOZI wa Marekani.

Taarifa iliyotolewa na ubalozi huo jana kwa vyombo vya habari ilisema pamoja na kukabiliwa na changamoto nyingi za kisheria, Melo na Jamii Forums, wameendelea kuwa mstari wa mbele katika kutetea uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania.

Taarifa hiyo ilisema Tanzania inajivunia historia kubwa iliyosheheni mchango mkubwa wa vyombo vya habari, kuanzia mchango wa Radio Tanzania Dar es Salaam katika ukombozi wa Afrika, kuimarisha umoja wa Afrika na kukuza amani na haki.

“Kutambuliwa kwa Maxence Melo na kutunukiwa kwake tuzo hii kunatukumbusha urithi huu muhimu wa historia ya nchi hii; urithi ambao unatishiwa pale ambapo matukio ya ukiukwaji wa haki, unyanyasaji na hata watu kupotea zinapogubika utamaduni wa maendeleo ya kijamii yanayosukumwa na vyombo vya habari,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza:

“Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania unatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kulinda urithi huu wa kihistoria kwa kuimarisha usalama wa waandishi wa habari na kutokomeza hali ya wale wanaowadhuru kutokuchukuliwa hatua zinazostahili.”

Habari Kubwa