Ubambikaji waibuka kesi Bil Msuya

17May 2018
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Ubambikaji waibuka kesi Bil Msuya

MSHTAKIWA wa nne katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa madini ya Tanzanite ‘Bilionea’ Erasto Msuya (43), Karim Kihundwa ambaye anadaiwa kuwa ndiye aliyefyatua risasi zilizomuua mfanyabiashara huyo,....

....Jana alibubujikwa na machozi karibu muda wote aliopewa kujitetea, huku akidai kwamba ametengenezewa kesi hiyo.

Kihundwa (37), aliyaeleza hayo mbele ya Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha wakati akitoa ushahidi wake wa kesi inayomkabili, akiongozwa na wakili Majura Magafu.

“Mheshimiwa Jaji, hii ni kesi ya kunitengenezea na ushahidi uliotolewa dhidi yangu ni wa uongo," alisema Kihundwa. "Sijawahi kutumia bunduki ya SMG ambayo ilitolewa hapa mahakamani na SSP (Mrakibu Mwandamizi wa Polisi) Lyimo ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Siha na wala sijui kutumia bunduki.

“Mimi huwa nazionaga (naziona) hizo SMG zikishikwa na askari na pia nimekuwa nikiziona kwenye movie (sinema) tu na wala sijawahi kuigusa kwa mkono Mheshimiwa.

"Naomba mahakama yako isizingatie ushahidi wa uongo uliotolewa na mahakama yako naomba iniachie huru niende kukusanya familia yangu ambayo imetawanyika baada ya mimi kupata matatizo haya.”

Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi 22, Agosti 7, 2013, majira ya saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Shahidi huyo wa kwanza wa utetezi, alipoulizwa na wakili Magafu kwamba anazungumziaje madai ya yeye kukiri kosa hilo katika maelezo yake aliyoyatoa kwa mlinzi wa amani, kwamba ndiye aliyefyatua risasi kumuua Bilionea Msuya, alijibu:

“Siyo kweli.

"Sijawahi kufanya hivyo... hiyo siku tukio linatokea mimi nilikuwa shambani kwangu West Kilimanjaro napalizi karoti na wala sijawahi kupitia mafunzo yoyote ya kijeshi nikashika bunduki. Sijawahi kupata mafunzo ya kutumia silaha, achilia mbali panga na shoka.”

Aliendelea kudai mahakamani hapo kwamba hajawahi kupelekwa hata Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Kaskazini iliyopo Arusha kuchukuliwa vipimo kwa ajili ya DNA (uchunguzi wa sampuli za vinasaba) na kwamba ushahidi uliotolewa kuwa alipelekwa huko ni uongo.

Jumatatu iliyopita Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi iliwaona washtakiwa sita kati ya saba katika kesi hiyo ya mauaji ya Bilionea Msuya kwamba wana kesi ya kujibu.

Aliyekuwa mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, Jalila Said (32) mkazi wa Babati aliachiwa huru baada ya uamuzi wa Jaji Maghimbi kueleza kwamba ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka haukumgusa kiasi cha kufanya awe na kesi ya kujibu.

Washtakiwa walioonekana wana kesi ya kujibu na wanaendelea kujitetea ni mshtakiwa wa kwanza Sharif Athuman (35), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, mshtakiwa wa pili Shaibu Saidi maarufu kama Mredii (42), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na mshtakiwa wa tatu Mussa Mangu (34), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu.

Wengine ni mshtakiwa wa tano Kihundwa, mkazi wa Lawate, Wilaya ya Siha, mshtakiwa wa sita Sadiki Jabir a.k.a Msudani (36), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, Wilaya ya Hai, na mshtakiwa wa saba Alli Musa maarufu Majeshi, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.

Kesi hiyo ya mauaji ya Bilionea Msuya ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi Oktoba 4, 2015.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo ambayo ni gumzo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, unaongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Abdala Chavula, akisaidiwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Omari Kibwana na Wakili wa Serikali, Kassim Nassir.

Mawakili wanaounda jopo la utetezi katika kesi hiyo ni Hudson Ndusyepo anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, Magafu anayemtetea mshtakiwa wa pili na wa tano, Wakili Emmanuel Safari anayemtetea mshtakiwa wa tatu na John Lundu anayewatetea washtakiwa wa sita na saba.

Hadi kufikia sasa, jumla ya mashahidi 27 wa upande wa mashtaka walishatoa ushahidi wao mahakamani hapo, huku maelezo ya mashahidi wengine wanne yakisoma kwa amri ya mahakama ambao walikuwa ni kati ya mashahidi 51 waliopangwa na Jamhuri kuijenga kesi hiyo.

Kesi hiyo itaendelea tena leo.

Habari Kubwa