Ubelgiji kuleta chanjo 115,200 corona leo

03Dec 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Ubelgiji kuleta chanjo 115,200 corona leo

SERIKALI leo inatarajia kupokea chanjo aina ya Johnson & Johnson dozi 115,200 kutoka Ubelgiji ili kuchangia kuongeza kasi ya kampeni ya kuchanja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ubalozi wa Ubelgiji na kuthibitishwa na serikali ya Tanzania, chanjo hizo zitachangia kuongeza kasi ya kampeni ya chanjo nchi nzima ili kulinda maisha na afya za Watanzania.

“Usambazaji wa chanjo hufanyika kupitia msambazaji wa kimataifa COVAX, na kuratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto ( UNICEF).

“Mchango huu ni sehemu ya ahadi ya awali ya Serikali ya Ubelgiji ya kusambaza angalau chanjo milioni nne kwa nchi za kipato cha kati na chini kufikia mwisho wa mwaka huu.”

Taarifa hiyo ilisema Ubelgiji imetekeleza ahadi hiyo na hadi kufikia sasa imetoa chanjo milioni tisa kupitia COVAX, pamoja na mchango wake wa kifedha wa EURO milioni 12.

Ilisema chanjo ya UVIKO-19 hupunguza hatari ya maambukizi pamoja na matatizo yake yanayoweza kuwa makubwa.

“Iwapo watu wengi iwezekanavyo Tanzania watapewa chanjo, kuenea kwa virusi hivyo kutazuilika.  Tunaipongeza serikali kwa kuzidisha kampeni za kuongeza uelewa ili kuwafahamisha wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kupata chanjo na kuwezesha kupatikana nchi nzima,” ilisema.

Taarifa hiyo ilisema upatikanaji wa chanjo ya UVIKO-19 Tanzania bado ni mdogo na ni chini ya wastani wa Afrika. “Kwa ombi la Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo, Meryame Kitir, mlengo wa nchi yetu wa kutoa michango baina ya nchi mbili utakuwa Afrika na hasa zaidi kwa nchi washirika wa Afrika, ambapo upatikanaji wa chanjo unakosekana sana,” ilifafanua.

Ilisema wakati Ubelgiji na nchi nyingi za Magharibi sasa zina viwango vya kuridhisha vya chanjo, kwa wastani barani Afrika karibu asilimia tano ya watu wamechanjwa.

Kaimu Mkuu wa Mawasiliano Idara ya Afya wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Catherine Sungura, alilithibitishia Nipashe kuwa serikali leo inatarajia kupokea msaada huo wa chanjo kutoka Ubelgiji.

Habari Kubwa