Ubovu barabara wasababisha wajawazito kujifungua njiani

23Jul 2021
Mary Mosha
SAME
Nipashe
Ubovu barabara wasababisha wajawazito kujifungua njiani

UBOVU wa barabara ya Miembe - Miamba - Ndungu Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro (kilomita 90), kumetajwa kusababisha wajawazito kujifungulia njiani na wengine kupoteza maisha kabla ya kufikishwa katika Hospitali ya Gonja. 

Vikwazo vingine vinavyosababishwa na ubovu wa barabara hiyo, ni kukosekana kwa magari ya abiria huku pikipiki zikishindwa kwenda baadhi ya maeneo hususani kipindi cha mvua kutokana na ubovu wa barabara hiyo. Ofisa Tarafa wa Gonja, Ibrahim Malisa, akielezea upungufu ya barabara hiyo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, alisema baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri wamekuwa wakisitisha safari za kufika maeneo hayo na kuwaacha wananchi wakiteseka kutokana na kuhofia kuharibiwa kwa vyombo vyao.

“Wajawazito na wagonjwa wa Kata ya Lugulu, Bombo, Vuje na Mtii kutokana na ubovu wa barabara hujifungulia njiani na wengine kupoteza maisha wakati wakipelekwa kwenye Hospitali ya Gonja kwa ajili ya matibabu, kutokana na ukorofi wa barabara hii,” alisema Malisa.

Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango, alisema kutokana na ubovu wa barabara hiyo, vijana na wanawake waliojiajiri kwenye kilimo na ujasiriamali wanashindwa kusafirisha mazao yao kwenye mikoa mbalimbali ya kibiashara ya badala yake kuozea shambani.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Lugulu, Mwanahawa Mzava, alisema kwa sasa wanakabiliwa na matatizo ya kipato kutokana na kukosa sehemu ya kuuza mazao yao baada ya kukomaa.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando, alisema serikali kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imeanza matengenezo ya barabara ya Miembe-Miamba Ndungu yenye urefu wa kilomita 90.

Alisema tayari mkandarasi yupo eneo la kazi na kuwa pamoja na kazi nyingine atalazimika kupasua miamba na kuondoa udongo ulioletwa barabarani.

Aidha, Naibu Waziri Waitara alisema serikali itahakikisha imetengeneza barabara hiyo kwa awamu ili wananchi wote wameweze kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi na kujipatia kipato. 

Habari Kubwa