Ubunge wa Lissu: Familia yaeleza kutuma barua 11

03Jul 2019
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Ubunge wa Lissu: Familia yaeleza kutuma barua 11

FAMILIA ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, imeweka bayana mawasiliano ya barua 11 walizoiandikia Ofisi ya Spika kuhusu hali ya kiongozi huyo anayeendelea na matibabu nchini Ubelgiji.

Wakili Alute Munghwai.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa kwenye moja ya blog, kaka yake Lissu, Wakili Alute Munghwai, alisema kauli ya Spika Job Ndugai kuwa hakuna mawasiliano yoyote kuhusu mbunge huyo siyo ya kweli, kwa kuwa mawasiliano yalifanyika kila wakati.

"Mwaka juzi na mwaka jana niliwasiliana na Ofisi ya Bunge kwa jumla ya barua 11 zilizoeleza suala la afya ya Lissu na alipopelekwa Ubelgiji vilevile tuliwataarifu na walijibu," alisema Munghwai.

Alisema Januari 10, mwaka jana, Ofisi ya Bunge ilimwandikia barua ikimtaarifu kuhusu kuteuliwa kwa madaktari bingwa watatu toka Hospitali ya Muhimbili ambao wangekwenda jijini Nairobi, kuchunguza afya ya Lissu na kuombwa kutoa ushirikiano.

"Nilijibu hii barua kwamba mgonjwa hayupo tena Nairobi, yupo Hospitali ya Leuven, Ubelgiji nikawapa na anuani ya hiyohospitali," alifafanua.

Vile vile, alisema barua nyingine ni ya Februari mosi, mwaka jana, kutoka Ofisi ya Bunge ikijumlisha kuwaofisi hiyo inawasiliana na Wizara ya Afya kwa hatuazaidi baada ya familia kumhamishia Lissu nchini Ubelgiji na kuahidi kuijulisha familia uamuzi utakaofikiwa na barua hiyo kunakiliwa kwa Spika na Lissu.

Akizungumzia madai ya kutokujaza fomu za maadili, wakili Munghwai alidai kuwa hicho ni kisingizio kipya kwa kuwa sababu za kutokujaza fomu hizo zinajulikana, ni kutokana na Lissu kuwa mgonjwa.

Lissu akinukuliwa katika kipande cha video na kufuatiwa na waraka aliousambaza kwenye mitandao ya kijamii, alisema sababu za kumvua ubunge ni za kuokoteza.

Waraka na kipande hicho cha video vimethibitishwa na Mkuu wa Idara ya Habari ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kusemadunia nzima inafuatilia masuala yanayoendelea nchini na inafahamu mahali alipotangu alipopigwa risasi Septemba 7, mwaka juzi.

"Sababu zilizotolewa ni za kuokoteza ili kujaribu kuhalalisha maamuzi haramu waliyoyafikia muda mrefu uliopita," alisikika Lissu kwenye kipande hicho cha video.

Vile vile, Mbunge huyo alisema anashangazwa na kauli ya Spika kwa kuwa viongozi mbalimbali akiwamo Makamu wa Raisaliyefika kumjulia hali katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Joseph Sokoine, alifika mara mbili katika Hospitali ya Chuo kikuu ya Leuven, kumuona.

Kwa mujibu wa Lissu, Bunge linajua alipo kwa kuwa Katibu wa Bunge Steven Kagaigai, amekuwa na mawasiliano rasmi na familia yake kwa ushahidi wa barua ikiwamo ya mwezi Machi, mwaka jana.

Alisema Katibu wa Bunge anadaiwa kumwandikia barua kaka yake kuhusu mgogoro wa Bunge kugharamia matibabu yake.

Membe anena

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema ameshangazwa na kitendo cha Tundu Lissu kuvuliwa ubunge.

“Kama Mtanzania na mimi nilishangazwa Lissu kuvuliwa ubunge, sasa  tusubiri aje, nina hakika kabisa ataenda mahakamani na kama kuna haki ataipata mahakamani,” alisema Membe.

Akizungumzia matukio mbalimbali ya watu kutekwa au kupotea, Membe aliwataka viongozi wakiwamo wa dini, vyama vya siasa na viongozi wastaafu kukemea suala hilo kwa kuwa ni utamaduni mpya aliodai unaiondolea Tanzania heshima duniani.

“Mimi naona huu ni utamaduni mpya ambao haukubaliki na ningependa kuchukua nafasi hii kusema tu kwamba suala la utekaji au watu kupotea linaweza kuiondolea nchi yetu heshima duniani,” alisema Membe.

Habari Kubwa