Ubungo kujazwa mamilioni ya jimbo

29Feb 2016
Elizaberth Zaya
Nipashe
Ubungo kujazwa mamilioni ya jimbo

MBUNGE wa Ubungo Saed Kubenea, amesema jimbo lake limepanga kupeleka Sh. milioni 200 kila Kata kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika Kata hizo.

MBUNGE wa Ubungo Saed Kubenea

Kubenea alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Umoja wa Wamiliki na Wazalishaji wa Unga wa Sembe na Dona (Uwawase) jijini Dar es Salam.

Alisema tayari fedha hizo za mfuko wa jimbo zimeshafika na kinachofanyika ni kupanga mikakati na kuchambua vipaumbele ambavyo fedha hizo zitaelekezwa.

Alisema uongozi wa jimbo hilo umepanga kuhakikisha unashughulikia kero na changamoto mbalimbali katika jimbo hilo, ikiwamo kuangalia namna ya kutumia fedha za mfuko huo kuwawezesha wananchi wake kiuchumi.

Mbali na kupeleka katika kila kata, alisema wamepanga kusaidia vikundi mbalimbali vya ujasiliamali katika miradi yao na hata ikiwezekana walipe kwa riba ndogo ili wananchi wote katika jimbo hilo wanufaike.

“Fedha za mfuko wa jimbo katika jimbo letu zimekwishafika. Tumepanga kila kata wapate kwa ajili ya maendeleo. Pia tunataka vikundi vitumie pesa hizo angalau hata kwa mkopo kwa riba ndogo ili izunguke na watu wote wapate.

Tunaamini kwa kufanya hivyo tutapunguza wategemezi katika jimbo letu,” alisema Kubenea.

Kadhalika, alisema anatarajia kupeleka hoja binafsi bungeni ili serikali ifikirie namna ya kuweka mpango wa kuwa inauza mahindi kwa vikundi vya uwekezaji vya ndani badala ya kuuza nje ya nchi.

Mbali na hilo, pia aliiomba Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuhakikisha inawapatia maeneo ya kuweka mashine za kusagia wazagishaji wa unga wa dona na sembe ili waondoke katikati ya mji.

Kwa upande wake, Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Jumanne Amiri, alisema wamepanga kukutana na wafanyabishara hao jumatatu ya wiki ijayo ili kujadiliana nao na kuona ni sehemu gani wanaweza kuwapatia maneo ya kuweka mashine zao za kusaga.

Habari Kubwa