Uchafu watafuna bil. 340/- kila mwaka

07Dec 2017
Paul Mabeja
Nipashe
Uchafu watafuna bil. 340/- kila mwaka

TANZANIA inapoteza Sh. bilioni 340 kila mwaka kutokana na kuwapo na huduma duni za usafi wa mazingira.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alipokuwa akikagua utekelezaji wa miradi ya usafi wa mazingira katika Kijiji cha Humekwa wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Mwalimu alisema kiasi hicho cha fedha kimekuwa kikipotea kila mwaka kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia hivi karibuni, kutokana na uchafu kuchangia mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu, minyoo na kuhala damu.

Alisema kiasi cha fedha nyingi kimekuwa kikitumika katika matibabu ya wagonjwa wanaotokana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu kutokana na idadi kubwa ya watu kutokuwa na vyoo.

“Tunatumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kutibia watu kutokana na magonjwa yatokanayo na uchafu, lakini pia watu wengi wanapoteza muda wao wa kushiriki shughuli za kiuchumi na kwenda kutafuta mapori kwa ajili ya kujisaidia kutokana na kukosa vyoo,” alisema Mwalimu.

Alisema asilimia 40 ya kaya nchini ndizo zenye vyoo bora, lakini asilimia 60 hawana kabisa vyoo na katika shule za msingi 100 takwimu zinaonyesha ni shule 28 zenye vyoo.

“Kama hapa mmeweza kuwa na vyoo kila kaya kila shule kwanini hali hii isiwezekane katika maeneo mengine, katika kampeni ya Tanzania ya viwanda hatuwezi kufanikiwa wakati idadi kubwa ya wananchi hawana vyoo,” alisema.

Awali,  Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Asha Amosi, akitoa taarifa fupi kwa waziri huyo alisema  wanashukuru ujio wa kampeni ya ‘Nipo tayari’ ambayo imesaidia ujenzi wa vyoo kwa kaya zote za kijiji hicho.

Alisema awali asilimia 54 ya wakazi wa kijiji hicho hawakuwa na vyoo, hivyo kujisaidia vichakani, lakini baada ya kupata elimu na kuwezeshwa kupitia mashirika kama Plan International na mradi wa Umata, kaya zote zimejenga vyoo.

“Hivi sasa tunashukuru kila kaya ina choo na watu wanatumia kikamilifu pamoja na hivi vibuyu chilizi kwa ajili ya kunawa mikono baaada ya kutoka chooni,” alisema Amosi. 

Habari Kubwa