Uchaguzi mdogo Temeke waiva

19Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Uchaguzi mdogo Temeke waiva

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa kata mbili utakaofanyika Januari 19, mwakani sambamba na uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Temeke na Kata 46 za Tanzania Bara uliotangazwa awali.


Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mbarouk Salim Mbarouk picha mtandao


Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mbarouk Salim Mbarouk, alizitaja kata hizo jana kuwa ni Mwanahina katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu  na Biturana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.  

“Fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya  Desemba 21 na 27, mwaka huu. Uteuzi wa wagombea utafanyika Desemba 27 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Desemba 28 hadi Januari 18, mwakani na siku ya uchaguzi itakuwa Januari 19,” alisema Jaji Mbarouk.


Aliongeza kuwa uchaguzi wa kata hizo ambao unafanyika kutokana na kujiuzulu uanachama kwa madiwani waliokuwapo awali, utafanyika pamoja na uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Temeke na Kata 46 za Tanzania Bara.

“Tume inapenda kuvikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kipindi chote cha Uchaguzi huu mdogo,” alisisitiza.


Alisema tume imetangaza nafasi hizo wazi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, aliiarifu tume uwapo wa nafasi wazi za madiwani katika kata hizo. 

“Kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa taarifa kwa umma kuhusu uwapo wa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata tajwa zilizoko katika Halmashauri za Meatu na Kibondo,” alisema Jaji Mbarouk.

Habari Kubwa