...Uchaguzi Spika wa Baraza Wawakilishi leo

08Nov 2020
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe Jumapili
...Uchaguzi Spika wa Baraza Wawakilishi leo

MKUTANO wa mwanzo wa Baraza la 10 la Wawakilishi unatarajiwa kuanza rasmi leo ukitarajiwa kuwapo na shughuli mbalimbali, ukiwamo uchaguzi wa spika wake.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa jana, Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Mselem, alisema uchaguzi wa spika wa baraza hilo utafayika leo.

Alisema waliochukua fomu ya kugombea nafasi hiyo ni watano akiwamo aliyekuwa Spika wa Baraza hilo, Zuberi Ali Maulid, kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aliwataja wengine kuwa ni Ali Makame kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Naima Salum Hamad kutoka chama cha UDP, Hamad Mohamed Ibrahim (UPDP) na Ameri Hassan Ameri kutoka Chama cha Demokrasia Makini.

Katibu huyo alisema baada ya uchaguzi huo, kutakuwa na kiapo cha Spika na kufuatiwa na kiapo cha uaminifu kwa wajumbe wa baraza hilo.

Alisema pia kutakuwa na uchaguzi wa naibu spika wa baraza hilo na kufuatiwa na uzinduzi wa baraza la 10.

Alisema Novemba 11 mwaka huu, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, atalifungua rasmi baraza hilo.

Katibu huyo alisema tayari wajumbe wa majimbo 50 ya uchaguzi ya Zanzibar waliotangazwa na Tume ya Uchahuzi Zanzibar wameshapewa taarifa kuhusu shughuli hiyo ambao ni kutoka vyama vya CCM na ACT-Wazalendo.

"Chama cha Mapinduzi tayari wameshajibu barua tuliyowapelekea kuhusu wajumbe wa baraza la wawakilishi kutokea chama hicho kuhudhuria vikao, lakini ACT hadi sasa bado hawajajibu barua yetu kuhusu ushiriki wa wajumbe wa baraza waliotangazwa na tume," alisema.

Hata hivyo, alisema wameshapokea wajumbe wa baraza la wawakilishi wa viti maalum kutoka CCM pekee ambao ni 18.

Katibu huyo aliwataka wananchi kuendelea kufuatilia shughuli mbalimbali za chombo hicho.

Habari Kubwa