'Uchaguzi wa ubunge ulikuwa na mizengwe'

03Mar 2016
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
'Uchaguzi wa ubunge ulikuwa na mizengwe'

ALIYEKUWA mgombea ubunge katika Jimbo la Longido kwa tiketi ya CCM, Dk. Steven Kiruswa, ameiambia Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuwa kura zilichezewa na kupunguzwa katika vituo 15 bila maelezo, huku zikitofautiana katika fomu ya wakala wake na za majumuisho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Sivangilwa Mwangesi, Dk. Kiruswa.

Akizungumza wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Sivangilwa Mwangesi, Dk. Kiruswa alidai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na mchezo mchafu.

Alisema katika kituo cha Sinoni Shuleni kituo namba 12, kwa mfano, kulikuwa na wapigakura 287 na waliopiga kura 233 lakini kura halali kwa mujibu wa fomu ya wakala wake ni 214, wakati fomu ya majumuisho ya msimamizi wa uchaguzi inaonyesha kura 19 hazimo katika kundi lolote.

Alisema pia kituo cha Naripi 2 waliojiandikisha 310, waliopiga kura 232 na kura halali 229 na kura moja imeharibika, lakini kwenye fomu ya majumuisho inaonyesha kura halali ni 228 na kura zilizoharibika mbili, hivyo kura moja haina maelezo.

Aidha katika kituo cha Engong’u 1, kura nne zilipotea bila maelezo, japo katika karatasi za wakala wake zimo ila karatasi za majumuisho zinapotea.

Dk. Steven alisema haelewi kura hizo zilichezewa kwa lengo gani na zilikuwa zikipotea bila maelezo, huku fomu za wakala wake zikionyeshakura zote, ila fomu za majumuisho zikionyesha upungufu wa baadhi ya kura bila maelezo.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana 2015, Nangole alitangazwa kuwa mshindi baada ya kupata kura 20,181 dhidi ya kura 19,361 za Dk.Steven Kiruswa wa CCM.

Miongoni wa hoja zilizopelekwa mahakamni hapo ni madai kuwa Onesmo ole Nangole (Chadema), alimtolea lugha ya kashfa wakati wa kampeni, Dk. Steven Kiruswa kuwa si Mmasai bali ni raia wa Marekani, kutokana na kufanya kazi nchini humo.

Pia hoja nyingine ni kwamba magari ya Chadema yalitumika kubeba masanduku ya kura kutoka kwenye vituo hadi halmashauri ya wilaya na uchaguzi na uchaguzi haukuwa huru na haki.

Katika kesi hiyo mdaiwa wa kwanza Nongole, wapili Msimamizi wauchaguzi na tatu mwanasheria Mkuu wa serikali.

Habari Kubwa