Uchunguzi malipo fedha za pembejeo mbioni kukamilika 

14Feb 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Uchunguzi malipo fedha za pembejeo mbioni kukamilika 

SERIKALI imesema vyombo vya uchunguzi viko katika hatua ya mwisho kumalizia uchunguzi wa fedha za mawakala wa pembejeo wanaoidai Sh. bilioni 35.
Mawakala hao ni waliosambaza pembejeo zikiwamo mbegu na mbolea katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, picha mtandao

Akizungumza jijini Dodoma jana, katika Kongamano la Tano la Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, alisema walikabidhi suala hilo kwa taasisi za kiuchunguzi baada ya kubaini uwapo wa utofauti ya deni linalodaiwa na mawakala hao.

"Uchunguzi utakapokamilika, taarifa itatolewa. Jambo hili baada ya serikali ya Rais John Magufuli kuingia madarakani, kama mnavyofahamu mwaka ukipita wa fedha madeni yote yanahamia Wizara ya Fedha, baada ya kuyachunguza madeni, tukakuta yana ukakasi kidogo, la kwanza bajeti iliyopitishwa mwaka ule ilikuwa Sh. bilioni 35 kwa ajili ya pembejeo zote nchini, lakini vocha zilizotengenezwa zilikuwa zaidi ya Sh. bilioni 70, ukakasi wa kwanza huo," alisema.

Mgumba alisema changamoto ya pili ni madeni yaliyowasilishwa wizarani kuwa zaidi ya Sh. bilioni 65 wakati bajeti ni Sh. bilioni 35.

“Kutokana na hali hiyo, tukaona tujiridhishe, tufanye uhakiki wa kina tuone tatizo ni nani waliotengeneza na  kujinufaisha, uchunguzi huo umefanyika na kila aina ya uchunguzi unaoujua wewe, na taarifa tulizokuwa nazo za awali kuna hujuma kubwa iliyofanyika kwa namna moja au nyingine wapo watumishi wa serikali, mawakala wenyewe na viongozi huko chini," alisema.

Naibu waziri huyo alisema mamlaka za kiuchunguzi ziko katika hatua za mwisho na watatoa mwongozo wa nani walitenda jinai hiyo na kuwachukulia hatua za kisheria.

“Pamoja na utofauti huo, tukawaambia mawakala wenyewe leteni tuone mnatudai shilingi ngapi, mawakala wakaleta wanadai Sh. bilioni 37 ilhali tulizoletewa mwanzo ni Sh. bilioni 65. Kwa namna yoyote hapo huwezi kulipa, tunaomba mawakala mwendelee kuwa na subira wakati serikali inaendelea kulisimamia jambo hili na hizi fedha za umma kwa umakini zaidi," alisema.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania, Jacquiline Mkindi, aliiomba serikali iendelee kufikiria kulipa madai sahihi ya wasambazaji wa pembejeo wanaoidai.

“Mwaka 2015/2016, kuna wasambazaji wa pembejeo nchini waliokuwa wanasambaza chini ya mfumo wa ruzuku ya mbolea, ambapo mpaka sasa wanadai na hawajalipwa fedha zao kiasi cha Sh. bilioni 36.9, tunaelewa kulikuwa na changamoto zilizotokana na mfumo huo, na serikali ilipitia madai hayo na kuwaadhibu watendaji wa serikali waliosababisha changamoto hizo na ubadhirifu uliotokea," alisema.

Akifungua kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Uwekezaji, Angellah Kairuki, alisema bado kuna changamoto ya uzalishaji wa mbegu bora nchini.
Mkutano huo umeandaliwa na Jukwaa la Wachambuzi wa Serikali wa Mifugo, Kilimo na Uvuvi ukiwa umewashirikisha washiriki zaidi ya 300 kwa lengo la kujadili changamoto na fursa zilizoko katika sekta ya kilimo.

Habari Kubwa