Uchunguzi waliosafirisha  mke, mume China waiva

12May 2018
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Uchunguzi waliosafirisha  mke, mume China waiva

MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imesema uchunguzi wa watu wanne wanaodaiwa kuhusika kuwasafirisha Watanzania wawili waliokamatwa nchini China na dawa za kulevya umefika pazuri.

Baraka Malali na Ashura Mussa.

Watanzania wawili ambao ni mke na mume, Baraka Malali na Ashura Mussa, walikamatwa Januari 19, mwaka huu kwenye uwanja wa ndege wa Baiyun Guangzhou, nchini China wakiwa wamemeza pipi 129 za dawa za kulevya.

Baada ya Watanzania hao kushikiliwa, mtoto wao wa miaka miwili na miezi tisa waliyesafiri naye alirudishwa Tanzania wakati wazazi wake wakisubiri taratibu za kufikishwa mahakamani nchini humo.

Nipashe ilizungumza na Kamshina wa Sheria wa DCEA, Edwin Kakolaki, ambaye alisema uchunguzi wa suala hilo unaendelea vizuri.

Alisema uchunguzi utachukua muda kwa kuwa kumekuwa kunaibuka na mambo mengine ambayo ni lazima wafuatilie kwa kina ili kukamilisha uchunguzi.

“Uchunguzi unakuwa na mambo mengi, uchunguzi wa muda mfupi ni kwa yule ambaye amekamatwa na ushahidi wa moja kwa moja, sasa kwa jambo hili ni taratibu za nchi na nchi katika kuwasiliana, hivyo kuna mambo mbalimbali tunayofuatilia ili kujiridhisha kama ni sahihi au la,” alisema na kuongeza:

“Katika suala hili unachunguza unafika katikati unaona kuna vitu vinahitajika, hivyo lazima usubiri mpaka upate taarifa kutoka China, lakini uchunguzi wetu unaendelea vizuri katika haya majina manne tutawapata waliohusika kuwasafirisha hawa Watanzania kupeleka ‘unga’ huko China,” alisema.

Wazazi hao baada ya kukamatwa Januari 19, mwaka huu walipimwa na kubainika wamemeza dawa za kulevya na kuwekwa katika chumba maalumu, Malali alitoa pipi 47 na Ashura pipi 82.Wakati wazazi hao wakiwa mahabusu, Serikali ya China iliwasiliana na Tanzania na kufanya utaratibu wa kumrudisha mtoto nchini huku wazazi hao wakisubiria hatma yao mahakamani.Watu wanaopatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya nchini China kwa kawaida hupewa adhabu ya kunyongwa mpaka kufa wakati kwa Tanzania hufungwa kifungo cha maisha kwa yeyote atakayekamatwa na ‘unga’ kuanzia gramu 20 na kuendelea.