Udhuru wakwamisha kesi ya Mbowe

14Nov 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Udhuru wakwamisha kesi ya Mbowe

KESI inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na wenzake wanane, itaendelea kesho kusikilizwa utetezi wa washtakiwa baada ya mawakili wa utetezi kuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu.

Wakili Dickson Matata, alidai kuwa Profesa Safari na Kibatala wako Mahakama Kuu wana kesi nyingine wanaendesha kwa siku mbili.

Matata alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba anayesikiliza kesi hiyo.

Kutokana na sababu hizo, alidai kuwa mawakili hao wameomba kesi hiyo iahirishwe hadi Novemba 26 hadi 29, mwaka huu, kuendelea na utetezi.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alipinga ahirisho la kesi hiyo kwa madai kuwa sababu zilizotolewa si za msingi na mawakili wanaodaiwa kuwa Mahakama Kuu wawasilishe uthibitisho.

Alidai kama mahakama itaridhia wakili Matata aendelee kuendesha shauri hilo au liendelee leo, kwa sababu washtakiwa hao wanawakilishwa na mawakili wengi.

Alitaja miongoni mwa mawakili hao kuwa ni John Mallya, Jeremiah Mtobesya, Marwa Magau na Omary Msemo na mahakama haijaelezwa mahali waliko.

Hakimu alimhoji wakili Matata aeleze waliko mawakili Mtobesya, Mallya, Magau na Msemo na akadai ana taarifa za mawakili watatu tu ambao ndiyo wanawawakilisha washtakiwa.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu Dk. Vincent Mashinji; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 13 likiwamo la kula njama kwa madai kuwa kati ya Februari 1 na 16, mwaka jana jijini Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Hakimu Simba alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa ushahidi wa utetezi na kwamba Mbowe ataendelea kuhojiwa na Jamhuri kesho.

Habari Kubwa