UDOM yawafunda waombaji vyuo vikuu

18Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
UDOM yawafunda waombaji vyuo vikuu

CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewataka wanaoomba kuingia vyuo vikuu kuhakikisha wanajaza fomu za kuomba program za masomo kwa kuzingatia sifa walizonazo kwa usahihi ili kuepusha malalamiko hapo baadaye kuwa hawakuchaguliwa wakati wana vigezo.

CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Faustine Bee, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika maonyesho ya vyuo vikuu yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Prof. Bee alisema aliwataka wanafunzi wa kidato cha sita ambao wanatarajia kuingia vyuo vikuu, wasome kwa umakini sifa zinazotakiwa kwenye chuo ndipo wajaze.

“Ukikosea kuomba programu ambayo haiendani na sifa ulizonazo mwanafunzi husika, utajikuta ameachwa na ukiachwa baadaye unalalamika.Tunasisitiza hili sana, wanafunzi wasome vizuri na wazingatie maelekezo ya vyuo wakati anaomba programu,” alisema.

Alisema katika maonyesho hayo, mbali ya kuonyesha programu zinazotolewa chuoni hapo, wanafanya udahili wa moja kwa moja.

“Kwa hiyo mwanafunzi anayekuja kwenye maonyesho atambue kuwa haji tu kwenye maonyesho, atapata fursa ya kudahiliwa moja kwa moja,” alisema.

Pia alisema wahadhiri na wanafunzi wa UDOM hushiriki katika kutoa huduma za jamii ambapo kupitia shule tanzu ya tiba UDOM kwa kushirikiana na hospitali ya Benjamin Mkapa walifanya upandikizaji figo kwa mara ya kwanza Tanzania.

“Tunaendelea kuimarisha nguvu na maarifa katika eneo hilo. Pia upo ushiriki wa wanafunzi wetu katika huduma nyingine za kijamii,” alisema na kuongeza:

“Lengo ni kuwajengea uwezo siyo wa maarifa darasani, pia uzoefu wa kutenda kwa vitendo ili wakimaliza wajiajiri, mfano ni mradi wa ufugaji nyuki.”