UDSM yadahilmara tano ya uwezo wake

15Apr 2019
Sanula Athanas
Dodoma
Nipashe
UDSM yadahilmara tano ya uwezo wake


CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimebainika kudahili wanafunzi kwa zaidi ya mara tano ya uwezo wake na kuibua hofu ya ubora wa elimu kinayotoa kwa wahitimu wake.


Changamoto hiyo imeibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, katika ripoti yake ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2017/18, iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma Jumatano.


Katika ripoti yake kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma, CAG Assad anabainisha kuwa mnamo mwaka 2016/17, UDSM ilidahili wanafunzi kwa zaidi ya asilimia 560 ikilinganishwa na mpango wake.


"Hii ina maana kuwa idadi ya wanafunzi waliodahiliwa ilipita uwezo wa chuo hicho. Zaidi ya hayo, nilibaini kuwa udahili haukuwa umetolewa taarifa kwa kiwango ambacho kila kitivo kilielewa idadi ya wanafunzi waliotakiwa kudahiliwa," anabainisha.


"Majadiliano na baadhi ya maofisa yalionyesha kuwa kiwango cha juu cha udahili huo hakikuwa na uwiano na rasilimali nyingine za chuo kama vile rasilimali watu na miundombinu ili kukidhi bila shida ongezeko hilo.

"
CAG Assad anabainisha kuwa ongezeko hilo kubwa la udahili linahatarisha ubora wa elimu watakaopata wahitimu, hivyo kuwa na athari ya muda mrefu kwa maendeleo ya taifa.


"Ninapendekeza UDSM itayarishe na kutekeleza mpango wa udahili ambao utatokana na tathmini ya mahitaji na uwezo wa chuo kikuu," Prof. Assad anasema.


Katika ripoti yake hiyo, CAG Assad pia anaushauri uongozi wa UDSM kuzingatia mkataba na kampuni hodhi ya Mlimani City ili kufuatilia kasi ya kukamilika kwa miradi iliyochelewa.


Anabainisha kuwa tarehe ya kukamilisha mradi wa Mlimani City siyo tena Septemba Mosi, 2006, kwa kuwa tarehe ya awali ilisogezwa mbele kupitia mkataba wa utendaji ambao umeainisha tarehe ya kumalizika kuwa ni Desemba 31, 2019.


"Wakati wa mkutano wa pamoja uliofanyika Aprili 20, 2017 kati ya UDSM, Kituo cha Uwekezaji (TIC) na Mlimani Holdings Ltd (MHL), MHL alisema kuwa ana nia ya kuweka bustani ya mimea Mlimani City kabla ya mwisho wa kipindi cha mkataba, lakini hapakuwa na mipango ya kujenga hoteli ya nyota nne.


"Hata hivyo, UDSM na TIC walimwomba MHL kutafakari upya suala la hoteli kulingana na mkataba uliopo na MHL aliahidi kufanya hivyo. UDSM tayari imeanzisha mchakato wa kurekebisha mkataba wa kukodisha ardhi," Prof. Assad anabainisha.


Habari Kubwa