UDSM yakutanisha wadau wa uchumi

10Aug 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
UDSM yakutanisha wadau wa uchumi

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimewakutanisha watafiti, watunga sera na wafanyabiashara ili kutafuta mbinu za kuhakikisha kila Mtanzania kwa nafasi yake aweze kuwa sehemu ya uchumi wa viwanda ifikapo 2025.

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Bonaventure Rutinwa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika kongamano la 18 la ujasiriamali na biashara ndogondogo Afrika lililowakutanisha wadau hao.

Kongamano hilo limeitishwa na Shule ya Biashara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS) na kushirikisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika kongamano hilo, Prof. Rutinwa alisema lina umuhimu kwa sababu serikali imejielekeza kwenye uchumi wa viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025.

“Kabla hujakimbia lazima utembee, hivyo kabla ya kufikiria viwanda vikubwa lazima uwe na vidogo ili vikue,” alisema.

Prof. Rutinwa alisema, utafiti unaonyesha nchi zilizoendelea karibuni zikiachwa zile zilizoendelea karne ya 19 wakati mapinduzi ya viwanda yakichukua nafasi yake, ziliendelea kutokana na sekta ya wajasiriamali wadogo na wakati.

Alisema faida mojawapo ya viwanda vidogo ni shirikishi na jumuishi.

“Nchi inaweza ikasema ina uchumi mkubwa kumbe ukakuta ni kwa sababu ina kampuni kubwa nne tu ambazo zinamilikiwa na asilimia mbili ya raia huku wakati wengine ni maskini, tunapoongelea uchumi wa wasajiriamali wadogo na wa kati tunazungumzia uchumi jumuishi na shirikishi ambao ndio umetukutanisha leo,” alisema.

Prof. Rutinwa alisema mkutano huo ni muhimu kwa sababu utatoa mbinu za kuhakikisha kila Mtanzania anaweza kuwa sehemu ya uchumi wa viwanda.

“Changamoto zipo tunapozungumzia uchumi shirikishi watu wanafikiri ili waweze kukua ni lazima uanze na kiwanda kikubwa, lakini ipo changamoto ya mitaji na sera, haya yote yataangaliwa leo,” alisema.

Alisema mara baada ya kongamano hilo mapendekezo yatakayotolewa yatawasilishwa serikalini na kwa wadau wengine.

Naye, Mkuu wa shule hiyo UDBS, Prof. Ulingeta Mbamba, alisema wameamua kufanya kongamano hilo ili kuwaleta wadau hao kujadili njia za kusonga mbele katika ukuzaji wa biashara na sekta ya wajasiriamali wadogo na wakati.

Kuhusu changamoto Prof. Mbamba alisema kila sekta ina changamoto zake ingawa maendeleo yanaendelea kupatikana.

“Na tukiangalia nguvu kubwa inayofanywa na serikali sekta ya viwanda imesaidia eneo hili kukua,” alisema.

Habari Kubwa