Ufafanuzi ndege zinazotua hifadhini

15Jan 2023
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Ufafanuzi ndege zinazotua hifadhini

WIZARA ya Maliasili na Utalii, imesema ndege zinazotua na kuruka katika viwanja ndani ya hifadhi zinasafirisha watalii kutoka Uwanja wa Ndege Dar es Salaam (JNIA), Kilimanjaro (KIA) na Abeid Amani Karume, Zanzibar.

Ufafanuzi huo unatokana na taarifa zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii kuwa ndege zinazoruka na kutua katika maeneo ya hifadhi zinasafirisha wanyamapori na rasilimali nyingine zinazolindwa na kuhifadhiwa kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kitengo cha mawasiliano cha wizara hiyo, taarifa hizo sio za kweli na wanawaomba wananchi kuzipuuza, kwa kuwa zina nia ovu ya kusababisha taharuki katika jamii.

“Tanzania ni nchi iliyobarikiwa vivutio vingi vya utalii zikiwamo hifadhi za taifa 22, mapori ya akiba 22, mapori tengefu 29, Hifadhi ya Ngorongoro, hifadhi za misitu, maeneo ya kihistoria na urithi wa dunia, hifadhi za bahari na fukwe, maziwa makuu, mito na maeneo mengine mengi ya asili.

“Maeneo haya ya vivutio yamekuwa yakitembelewa na watalii wa aina mbalimbali na kuliingizia taifa fedha za kigeni pamoja na kuzalisha fursa za ajira,” ilisema.

Taarifa hiyo iliendelea kufafanua kuwa watalii wengi wanatembelea Tanzania kutokana na juhudi kubwa za kutangaza utalii zilizofanyika ambazo zimekuwa kichocheo cha shughuli mbalimbali zikiwamo za utalii wa picha, safari za parachute, kutembea nyikani, ufukweni na kupanda milima.

Aidha, ilieleza kutokana na umuhimu wa shughuli hizo, serikali imefanya maboresho ya kukarabati miundombinu ya utalii vikiwamo viwanja vya ndege, barabara na miundombinu mingine muhimu katika maeneo ya hifadhi, ili kuwezesha uendelevu wa shughuli za uhifadhi.

Wizara imewahakikishia Watanzania kuwa viwanja vyote vya ndege katika maeneo ya hifadhi viko salama na vinatumika kwa shughuli za usafirishaji wa watalii wanaotoka katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Wizara iko makini kuhakikisha matumizi sahihi ya viwanja hivyo kwa wageni wote wanaoingia na kutoka katika maeneo ya hifadhi. Tunawaomba wananchi muwe watulivu na kuwa makini na watu wanaotoa taarifa za upotoshaji na za kichochezi zisizo rasmi kuhusu ndege na matumizi ya viwanja hivyo,” ilisisitiza.

Pia wizara iliwasisitiza wananchi wanapoona matumizi yasiyo sahihi wasisite kutoa taarifa kwenye vituo vyao vya uhifadhi, polisi au ofisi za serikali zilizo katika maeneo yao, ili kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za taifa.

Habari Kubwa