Ufaransa kusaidia TZ kupambana na magonjwa

08Nov 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Ufaransa kusaidia TZ kupambana na magonjwa

BALOZI wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier, amesema serikali yake imetoa kipaumbele kupambana na magonjwa makubwa nchini Tanzania ili kupunguza idadi ya vifo.

BALOZI wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier, picha mtandao

Alisema hayo katika uzinduzi wa Siku ya Afya ya Kifaransa juzi na kuungwa mkono na kampuni za Ufaransa zinazoshughulika na masuala ya afya, Sanofi na Biomerieux.

“Ningependa kuweka msisitizo katika majukwaa ya kimataifa, masuala yanayohusu afya tunayapa kipaumbele kwa Ufaransa na nchi nyingine zote za Umoja wa Ulaya,” alisema Clavier.

Alisema wataangalia mikakati tofauti katika nchi jinsi asasi za kiraia zilivyojikita kwenye sekta ya afya kwa ajili ya kupunguza vifo na magonjwa makubwa, kusambaza vifaa na kutoa elimu kuhusu afya kutokana na kupewa kipaumbele cha kwanza kwa magonjwa ya milipuko duniani.

Alisema suala la kudhibiti vifo vya wajawazito wamelipa kipaumbele kutokana na kinamama kufariki wakati wa kujifungua.

Alisema moja ya sababu ya vifo hivyo ni maambukizi ya magonjwa kwa wajawazito na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza.
Pia asilimia 80 ya wagonjwa kuchelewa kugundua ugonjwa na wataalamu wa afya kuwa changamoto.

Clavier alisema Serikali ya Ufaransa kwa kushirikiana na wawakilishi kutoka Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), wameweka kipaumbele suala la afya nchini.

Alisema mkakati wao ni kuimarisha vifaa vya kutoa huduma na mafunzo kwa wataalamu wa afya ili kusaidia jamii kuwa na uelewa wa kujua dalili za mwanzo za ugonjwa wa saratani na utafiti katika magonjwa hayo.

Katika maendeleo ya sera ya afya, alisema dhumuni lao ni kuendeleza upatikanaji wa dawa.

Meneja wa kampuni ya BioMerieux inayojihusisha na afya, Jacqueline Karachi, alisema ni muhimu kuwa na takwimu sahihi za magonjwa ili yaweze kutolewa tiba sahihi.

Alisema kuna baadhi ya wagonjwa huanza kunywa dawa kabla ya kugundua anasumbuliwa na ugonjwa gani.

“Wananchi wanajikuta wanaingia gharama kubwa kujitibu ugonjwa ambao haupo ni muhimu kufanyiwa uchunguzi na wataalamu kwa kuwa unapoendelea kunywa dawa hazifanyi kazi mwilini,” alisisitiza.

Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk. Siana Nkya, alisema kwa sasa wanafanya utafiti wa kupata tiba ya ugonjwa wa selimundo.

Alisema jamii nyingi hazina uelewa wa matibabu kwa mtoto ambaye anazaliwa na selimundo ingawa maisha yao hayazidi umri wa miaka mitano na kufariki.

Dk. Nkya alishauri kuanzishwa programu maalum ya kuwapima watoto wanapozaliwa ili kujua kama wamezaliwa na ugonjwa huo waanze kupatiwa tiba mapema ili iwasaidie kuongeza umri wa kuishi.

Habari Kubwa