Ufaransa yaipa Tanzania bil. 600/- za miradi mitatu

30Jun 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Ufaransa yaipa Tanzania bil. 600/- za miradi mitatu

SERIKALI ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) zimesaini mikataba ya mkopo ya kutekeleza miradi mitatu ya kipaumbele ya umeme na maji inayokadiriwa kufikia Sh. bilioni 600.

Mikataba hiyo ilisainiwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, kwa niaba ya serikali na Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier na Mkurugenzi Mkazi wa AFD, Stéphanie Mouen.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, James aliainisha miradi hiyo ni wa usambazaji umeme vijijini ambao utagharimu Euro milioni 100 (sawa na Sh. bilioni 257.64) na utasambazwa katika mikoa 16 ya Tanzania Bara.

Alisema una lengo la kuhamasisha ukuaji mpana wa uchumi, kuongeza vipato vya watu wa vijijini na kuongeza ubora wa maisha na ustawi wa jamii vijijini.

“Utajikita katika kuunganisha umeme majumbani, taasisi, vituo vya usambazaji wa maji na biashara, ambapo matarajio ni kufikia makazi 3,788 katika vijiji 1,304 kwenye mikoa 16 ya Tanzania Bara.

“Utahusisha kujenga njia za umeme zinazofikia kilometa 3,949.5, kuweka transfoma 1,291 zenye ukubwa wa kVA 50, transfoma 876 za kVA 10, transfoma 464 za kVA 200 na kuunganisha wateja 81,957.”

James alitaja mradi wa pili kuwa ni wa umeme wa kuunganisha Tanzania na Zambia ambao utagharimu Euro milioni 100 (sawa na Sh. bilioni 257.64).

Alisema mradi huo ni kwa ajili ya kuchangia uunganishaji wa mashirika ya umeme ya kusini mwa Afrika na mashirika ya umeme ya Afrika Mashariki.

Alisema unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400 na vituo vya kupoozea umeme katika ushoroba wa Iringa-Kisada -Mbeya -Tunduma - Sumbawanga.

Alitaja mradi wa tatu ni wa kazi za nyongeza kwenye mradi wa majisafi na majitaka katika miji inayozunguka Ziwa Victoria ambazo zitagharimu Euro milioni 30 (sawa na Sh. bilioni 77.29) na itahusisha maeneo ya Buhongwa, Kisesa, Buswelu katika jijini la Mwanza.

Alisema kiwango cha uzalishaji wa maji katika Jiji la Mwanza kupitia chanzo cha Kusini mwa jiji hilo ambacho ni mtambo wa kuzalisha maji wa Butimba kinatarajiwa kuwa mita za ujazo 20,000 kwa siku.

“Kupitia mkopo huu wa nyongeza mtambo huu wa kuzalisha maji utaongezewa uwezo wa kuzalisha kati ya mita za ujazo 40,000 hadi 45,000 kwa siku, na kuwezesha kupatikana kwa maji ya kutosha kwa maeneo yaliyotajwa ambayo hayakuwapo kwenye mradi hapo awali,” alisema.

James alibainisha kuwa miradi hiyo yote iliyosainiwa inawiana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025, ambayo inaongoza juhudi za kuleta maendeleo nchini.

Alisema kwa sasa inatekelezwa kupitia Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II) 2016/17 – 2020/21.

“Napenda kumshukuru Rais John Magufuli kwa kuendelea kudumisha uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Ufaransa, uhusiano huu umefanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwamo sekta za maji na nishati,” alisema.

Mkurugenzi wa AFD, Mouen alisema Ufaransa imedhamiria kuisaidia Tanzania katika jitihada za kufikia uchumi wa kati wa maendeleo.

Alisema mwaka 2019 ulikuwa wa historia ambapo Euro milioni 170 zilipitishwa na shirika hilo kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania na Euro milioni 300 nazo zimeshasainiwa.

Alisema wanaamini mwaka 2021 utakuwa ni wa utekelezaji wa miradi yote muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Naye Balozi Clavier alisema kwa miaka hiyo miwili wameona Ufaransa na Tanzania zikisaini makubaliano ya mikopo mikubwa ya kusaidia miradi ya maendeleo.

Habari Kubwa