Ufaransa yajitosa Stiegler’s Gorge

19Mar 2018
Gwamaka Alipipi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ufaransa yajitosa Stiegler’s Gorge

SERIKALI ya Ufaransa imesema iko tayari kuwekeza katika mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler's Gorge pamoja sekta za kilimo, maji na usafirishaji nchini.

Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier.

Hatua hiyo imetokana na nchi hiyo kuongeza bajeti ya uwekezaji nchini kutoka Euro milioni 50 (Sh. bilioni 138.25) mwaka jana hadi Euro milioni 100 (Sh. bilioni 276.5) mwaka huu.

Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier, ndiye aliyeyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati ya Ufaransa katika uwekezaji Tanzania wakati wa hafla ya chakula cha jioni jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

“Ufaransa imetambua jitihada zinazofanywa na serikali ya Rais John Magufuli, hivyo itaongeza uwekezaji hususani katika maji, nishati na usafirishaji,” alisema Balozi Clavier.

Aliongeza kuwa mbali ya uwekezaji katika sekta hizo, Ufaransa pia itatoa kipaumbele katika kuwafadhili wanafunzi wa Tanzania wanaosoma elimu ya juu kwenda kusoma Ufaransa.

Katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, alisema Ufaransa imetambua Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 inayosisitiza utoaji wa maji safi kwa wananchi mijini na vijijini.

Alisema kutokana na kutambua huko, imesema itafanya uwekezaji katika sekta za nishati hususani upanuzi wa mitambo ya kutoa umeme ya Hale.

Dk. Akwilapo alisema katika sekta ya elimu, Ufaransa imeahidi kuongeza nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma elimu ya juu.

Alisema awali kulikuwapo na matatizo ya wanafunzi wa Kitanzania kwenda kusoma Ufaransa kutokana na kutofahamu lugha ya Kifaransa, lakini kwa sasa kuna vyuo nchini humo vinavyotoa mafunzo kwa lugha ya Kiingereza.

"Sasa tutatumia fursa hiyo kupeleka wanafunzi wengi, kwa sababu awali tulikuwa tunapeleka wanafunzi katika vyuo vikuu vya China, Urusi, Canada na India," alisema Dk. Akwilapo.

Aliongeza kuwa kutokana na uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili, Tanzania itatumia nafasi hiyo kuiomba Ufaransa kuongeza idadi ya madaktari bingwa wa dawa za usingizi katika Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) Kampasi ya Mloganzila.

"Tuna madaktari wachache hususani madaktasi wa dawa za usingizi, wapo wachache sana, hivyo tukipata nafasi tutawaomba watusaidie," alisema.

Alibainisha kuwa Hospitali ya Mloganzila wanashindwa kufanya operesheni kwa sababu hawana wataalamu wa usingizi.

Alisema tayari maprofesa wa Ufaransa na Tanzania wamekutana kuainisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano na baada ya hapo watatoa mrejesho kuhusu namna walivyokubalina.

 

Habari Kubwa