Ugonjwa hatari usiofahamika kwa wengi watikisa Muhimbili

18Oct 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Ugonjwa hatari usiofahamika kwa wengi watikisa Muhimbili
  • *Husababisha maradhi mengine *Muhimbili watibu watano kila wiki *Madaktari bingwa wataja chanzo *Matibabu yahusisha kukata utumbo

KUTOKWA haja kubwa bila kujijua ni ugonjwa unaosababishwa na kukosa seli kwenye utumbo mkubwa zinazosaidia kusukuma haja kubwa kuitoa ndani ya utumbo.

Wataalamu wa masuala ya tiba za binadamu wanauita 'Hisrschospron’s desease'. Ni ugonjwa usiofahamika kwa watu wengi, lakini madaktari bingwa wanabainisha kuwa unawakabili watoto wengi nchini.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zaituni Bohari, anasema ugonjwa huo umeonekana kwa watu wengi kama siyo tatizo kwa watoto nchini bali unachukuliwa kama tabia.

Anasema watoto wengi wamekuwa wakichapwa na wazazi na walimu kwa muda mrefu bila kujua kuwa wanawaonea kwa sababu hilo ni tatizo lilipo nje ya uwezo wao.

"Watoto wengi wanapata shida ya kuchapwa fimbo na wazazi wao na kupewa adhabu shuleni kwa kosa la kujinyea wakati suala hilo lipo nje ya uwezo wao,” anasema Dk. Bohari.

Mtaalamu huyo anasema chanzo cha ugonjwa huo ni kukosekana kwa seli katika sehemu ya utumbo mkubwa unaopitisha haja kubwa, hali inayomfanya mtoto kushindwa kuzuia kinyesi kinapokuwa kinatoka.

Anafafanua kuwa kinyesi kikiwa kinashuka kwenye utumbo mkubwa ambao una seli, kinakwama eneo la utumbo ambalo halina seli na hivyo kumfanya mtoto ashindwe kupata choo kwa muda mwafaka.

Dk. Bohari anasema wakati kinyesi kinakamuliwa na kushuka katika eneo la utumbo lenye seli, huwa kinakwama eneo ambalo hakuna seli na hivyo kujirundika eneo hilo.

Anasema kinyesi kinaendelea kujirundika kwa muda mrefu na kusababisha tumbo kujaa na matokeo yake kinyesi kinashindwa kujisikuma kutoka nje na badala yake kuanza kutoka kidogo kidogo.

“Matokeo yake ni kwamba kikianza kushuka kidogo kidogo, mtoto anaanza kuchafua nguo bila kujijua na hivyo kuonekana amejinyea,” anasema Dk. Bohari.

Anasema wazazi wengi wanakuwa hawafahamu kama hilo ni tatizo kwa sababu watoto wanakuwa hawapati kinyesi kwa muda mrefu.

Mtaalamu huyo anabainisha kuwa mwanzo wa tatizo hilo ni pale mtoto anapozaliwa, lakini anachelewa kupata kinyesi cha kijani kwa mara ya kwanza ndani ya saa 24 na kupata ndani ya saa 48.

“Wazazi wakishajifungua, tunawaambia watoto lazima wapate kinyesi cha kijani ndani ya saa 24 na wanapochelewa kukipata, ni tatizo.

"Lakini, wazazi wanakaa kimya badala ya kurudi hospitali ili mtoto apatiwe matibabu, wanaanza kushauriana kuwapa maji au mafuta ili kulainisha kitoke na kweli kinatoka,” anasema Dk. Bohari.

MATIBABU YAKE

Dk. Bohari anasema wanapompokea mtoto mwenye tatizo hilo, wanaanza kwa kumpa dawa za kulainisha 'choo' na zingine wanamwekea kwenye mfumo wa haja kubwa.

Anasema mtoto kuwa na tatizo hilo humsababisha kupata homa za mara kwa mara, malaria na kupata choo kigumu kama mavi ya mbuzi.

Anafafanua kuwa baada ya kupewa dawa za kulainisha choo, humtengenezea sehemu ya kutolea haja kubwa eneo la ubavuni kwa ajili ya kujisaidia kwa muda akisubiri kufanyiwa upasuaji mkubwa.

Anasema kuwa katika hatua za awali ya kubaini tatizo, wanakata nyama ya eneo la kutolea haja kubwa kwa ajili ya kupima kujua kama hana seli hizo.

Dk. Bohari anasema baada ya kukata nyama, sampuli hiyo hupelekwa maabara kwa ajili ya kupimwa ili kubaini kama hana seli.

Anasema wakibaini tatizo, wanakata utumbo wote ambao hauna seli na kuunganisha kwa kuvuta utumbo mzuri wenye seli hadi karibu na sehemu ya haja kubwa.

Anasema wakishaunganisha utumbo wenye seli na kuondoa ule mbaya, mtoto anaweza kuendelea kupata haja kubwa kama kawaida bila shida yoyote.

WAGONJWA 20 KWA MWEZI

Dk. Bohari anabainisha kuwa kuna wastani wa watoto wanaofiokishwa Muhimbili kupata matibabu ya ugonjwa huo kila wiki na kati yao, wawili hufanyiwa upasuaji.

Anasema upasuaji wanaofanya kwa watoto ni mkubwa, hivyo hulazimika kuwafanyia upasuaji wawili tu kwa kila wiki ili kutoa fursa za upasuji kwa wagonjwa wa magonjwa mengine.

"Matibabu haya ya mtoto kwa hatua zote yanaweza kuchukua mwaka mmoja hadi kupona kabisa tatizo hili," anabainisha mtaalamu huyo wa Muhimbili.

Daktari huyo anawasihi wazazi 'kutochukulia poa' tatizo la mtoto kukosa choo, hivyo wanapaswa kwenda kituo cha afya pindi wanapoona hali ili kufanyiwa vipimo vitakavyobaini tatizo.

Habari Kubwa