Ugonjwa wa fistula bado tatizo nchini

22May 2022
Yasmine Protace
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Ugonjwa wa fistula bado tatizo nchini

​​​​​​​MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Rashid Mfaume, amesema ugonjwa wa fistula ya uzazi bado ni tatizo nchini na kwamba zaidi ya watu milioni mbili duniani wanaishi na ugonjwa huo.

Amesema mbali na idadi hiyo pia kuna visa takribani laki moja vilivyoripotiwa duniani kuwa na ugonjwa huo.

Dk. Mfaume aliyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Fistula.

Maadhimisho hayo yalifanyika Hospitali ya CCBRT, Jijini Dar es Salaam, kwamba alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala.

Kutokana na tatizo hilo, Dk. Mfaume alisema elimu inapaswa kuendelea kutolewa na kwamba ugonjwa huo umekuwa ukiwatesa watu ambao wamekuwa wakichelewa kupata matibabu.

Aliipongeza Hospitali ya CCBRT kwa kutoa matibabu bure kwa wagonjwa wa fistula ikiwamo kuwapatia chakula na nauli za kuwatoa mikoani na kuwaleta katika hospitali yao ili wapate matibabu.

Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT, Brenda Msangi, alisema ugonjwa wa fistula unatibika, hivyo jamii inapokuwa na wagonjwa hao wawapeleke hospitalini kupata matibabu.

Alisema kesho Tanzania itaungana na  huungana na nchi zingine duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza fistula ya uzazi.

"Huu ni mwaka wa 10 tangu tulipoanza kuungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hii mwaka 2013," alisema.

Msangi alisema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Tokomeza Fistula, Wekeza, Imarisha Huduma za Afya na Wezesha Jamii’.

Aliongeza kuwa kaulimbiu hiyo inamaanisha kuwekeza na kuimarisha huduma za afya.

Alisema CCBRT ikishirikiana na wadau mbalimbali, ikiwamo serikali, wametekeleza kaulimbiu hiyo kwa kufanya uwekezaji mkubwa kwa kujenga kitengo kipya cha afya ya mama na mtoto ambacho kinalenga kuwahudumia kinamama wenye historia ya fistula.

Msangi pia alisema huwaudumia watu wenye ulemavu, mabinti wanaopata mimba za utotoni, lengo ni kuzuia fistula mpya, pamoja na kuondoa vifo vya mama na mtoto.

Aliongeza kuwa tangu kuanza kwa mapambano dhidi ya fistula mwaka 2003, wamepiga hatua kitaifa katika kutoa matibabu ya fistula kwa maelfu ya kinamama wenye tatizo hilo, kwamba zaidi ya kinamama 17,500 wamepatiwa matibabu hospitalini hapo.

Habari Kubwa