Uhaba wa damu bado tatizo kubwa

19Mar 2017
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Uhaba wa damu bado tatizo kubwa

SERIKALI imekiri kuwa uchagiaji wa damu salama bado ni tatizo kwa kuwa kiasi kinachopatikana nchini kote ni asilimia 60 tu.

DAMU.

Kutokana na hali hiyo, serikali imeyataka madhehebu ya dini, taasisi za umma na binafsi, watu binafsi kuchangia damu, ili kuokoa maisha hususan ya watoto na kinamama.

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Mohamed Kambi, Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati waumini wa kanisa la Waadventisti Wasabato wakichangia damu, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi, alisema kwa sasa kuna mahitaji makubwa ya damu hivyo jamii inapaswa kujitolea ili kuokoa maisha ya wagonjwa hususan kinamama na watoto.

Alisema mahitaji ya damu kwa mwaka nchini ni lita 300,000 na kwamba uwezo wa ukusanyaji damu ni lita 200,000 sawa na asilimia 60, hivyo serikali imeendelea kutoa hamasa, ili jamii ichangie damu kwa hiari ili kukabiliana na upungufu uliopo.

“Damu inachangiwa kwa hiari unapochangia unawasadia zaidi wenye mahitaji makubwa kinamama na watoto, pia majeruhi, wagonjwa, serikali inasisitiza kuwa damu haiuzwi inatolewa bure, vijana hawa 700 wakiandventisti kuchangia damu leo (jana ni mfano wa kuigwa),” alisema Prof. Kambi.

Alisema damu ambayo anawekwa kwa wagonjwa ni salama, kutokana na kupimwa kwanza ili kubaini kama ina maambukizi ya magonjwa mbalimbali kama kaswende na homa ya ini.

Meneja wa Kanda ya Mashariki kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS), Dk. Aveline Mgasa, alisema matarajio ya ukusanyaji wa damu jana yalikuwa chupa 1,000, na kwamba hamasa ya uchangiaji imeendelea kukua ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Alisema mwaka jana ilikusanywa lita 190,000 nchi nzima, ikilinganishwa na mwaka 2015 ilikusanywa lita 140,000.

“Hamasa inaendelea kukua hivyo tunawaomba Watanzania waendelee kuchangia damu ili kuwasaidia wenye mahitaji ambao ni kinamama na watoto,” alisema Dk. Mgasa.

Habari Kubwa