Uhaba wa maji kuikumba Dar

16Sep 2021
Frank Monyo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Uhaba wa maji kuikumba Dar

BODI ya Bonde la Wami/Ruvu imesitisha kutoa vibali vipya vya uvunaji maji katika bonde hilo pamoja na kuwataka wananchi kuacha mara moja kufanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya mito.

Kaimu Mkurugenzi wa Bonde la Wami/Ruvu, Elibariki Mmasi.

Hatua hiyo imekuja baada ya kupungua kwa kina cha maji, katika chanzo hicho kufuatia upungufu wa mvua kwa msimu huu na ujao pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.

Kaimu Mkurugenzi wa Bonde la Wami/Ruvu, Elibariki Mmasi, akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kutembelea chanzo hicho, alisema kina cha maji kimepungua kulinganishwa na Septemba mwaka jana, kilipokuwa na kina cha milimita 12,500 hadi kufikia 7,500 kwa sasa.

Alisema Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inachukua milimita 5,000 kwa sekunde kutoka katika mto huo na kusisitiza kuwa kama hali ya ukame ikiendelea hivyo, mto huo utakauka na kusababisha mitambo ya DAWASA kupungua uwezo wa uzalishaji maji na kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

Alisema hivi sasa DAWASA na wateja wengine wanaotumia maji ya mto huo katika juhudi za kuhakikisha mitambo yao inakuwa na maji wanatumia mifuko ya sandarusi, maarufu viroba, kuongoza maji kwenda kwenye mitambo yao ili kukabiliana na upungufu huo.

DAWASA kwa kiasi kikubwa wanategemea maji kutoka mto huo kuhudumia wateja wake majumbani pamoja na viwanda vikubwa na vidogo vya Dar es Salaam na Pwani kutumia maji ya mto huo.

"Kuna kampuni nyingi zimekuja kwetu kuomba kibali cha matumizi ya maji, tumekataa kwa ajili ya kuyalinda maji, kwa ajili ya watumiaji wa maji majumbani hata kama ni kidogo.

Pia tumesitisha shughuli zote za umwagiliaji kwani uwezo wa mto wetu hauwezi kukidhi shughuli hiyo, tumewashauri wajenge visima, kwa ajili ya kumwagilia katika kipindi hiki cha kiangazi.

"Bodi ya Bonde la Wami/Ruvu haiwezi kuruhusu kuendelea shughuli za kibinadamu wakati mazingira ya kulinda vyanzo vya maji tumewawekea shughuli mbadala ambazo watu wanaweza kufanya katika kipindi cha kiangazi kama ufugaji nyuki, kwa hali hiyo hakuna kibali chochote kitakachotolewa kwa sasa, ili kuchukua tahadhari siku zijazo," alisema Mmasi.

Alisema bodi hiyo itaanza operesheni kali ya kubaini watu au kampuni, ambazo zinatumia maji ya mto huo bila kuwa na kibali na kuwachukulia hatua za kisheria, ili kudhibiti hali hiyo.

Kaimu Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kilichobaki kwa sasa ni mategemeo ya mvua kunyesha mapema lakini ikichelewa, wananchi wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani watapata maji kidogo.

Alifafanua kuwa shughuli inayofanyika kwa sasa na bonde hilo ni kudhibiti maji kutoka katika chanzo hicho kwa baadhi ya mito kuchepushwa ovyo pamoja na ujenzi wa Bwawa la Dunda, ambalo kukitokea uhaba wa maji, litakuwa linatumiika.

"Utunzaji wa vyanzo vya maji ni jukumu la wote kwani kuacha vyanzo hivyo vitatumika kiholela madhara yake ni makubwa sana.

"Kuna faini zipo kutokana na sheria zilizowekwa katika utunzaji wa vyanzo maji kuanzia laki tatu (300,000/-) hadi Sh. milioni 50 na baada ya hapo kufunguliwa mashtaka mahakamani," alionya.

Kaimu Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa wananchi hususani wa Dar es Salaam na Pwani kutumia maji kwa uangalifu ili kukabiliana adha hiyo.

Mwezi huu Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa tahadhari ya kuwapo ukame katika mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka, hali iliyotokea pia mwaka 2005, yaani miaka 16 iliyopita.

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa TMA, Dk. Hamza Kabelwa, alisema mifumo ya hali ya hewa inayotumika kuangalia mwenendo wa hali ya hewa imeonyesha kuwapo kwa kiwango kidogo cha mvua mpaka chini ya wastani kwa maeneo hayo.

Aliitaja mikoa inayotarajiwa kuwa na upungufu wa mvua kuwa ni Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Pwani katika kisiwa cha Mafia, Unguja na Pemba.

"Lakini  kwa upande wa Sekta za Nishati, Maji na Madini, tunatarajia kuwapo kwa hali ya ukame utakaofanya vyanzo mbalimbali vya maji kukauka, hivyo wahusika wanapaswa kuchukua tahadhari kwa athari zitakazojitokeza," alisema Kabelwa.